
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuna Watu walisema Rais amekosea kuteua mtu kutoka chama kingine.
Samia amesema hayo leo Jumatano, Juni 2, 2021 wakati akiwaapisha Makatibu Tawala wa Mikoa na viongozi mbalimbali aliyowateua hivi karibuni, katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
“Wakuu wa mikoa waliowekewa Ma-RAS wanawake, hawa ni wafanyakazi, maofisa na wasomi kama mlivyo nyie, sasa mkienda huko ‘wewe usinibabaishe si ni mwanamke tu’ aliyekwambia nani mwanamke ni TU?
“Wewe ulizaliwa na nani, ulikuzwa na nani na sasa unatunzwa na nani, aliyekufanya uitwe baba ni nani? Mambo ya kudharauliana yasiwepo. Nilishasema kila Mtanzania bila kujali Chama, Dini ataingia na kuchangia nchi hii.
“Kwa mkoa wa Iringa tuna-experience ya Kilimanjaro tulipomuweka Mghwira walimpa shida sana ma-DC wake, mara wewe siyo mwenzetu, aliyekuleta hapa amekosea, Rais huwa hakosei tunawavuta hao kutoka vyama vingine waingie nao ni Watanzania.
“Muende mkafanye kazi wote sawa kwa sawa, mkaheshimiane, mjenge ushirikiano na mpendane na ninaposema mpendane Wakuu wa mikoa na Ma- RAS wanawake kwa wanaume sikusudii yale, mkapendane kwenye kazi,” amesema Rais Samia.