
MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Iringa, Petronel Mwanisawa (22) amefariki dunia kwa kunyongwa na mpenzi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtuhumiwa, Prudence Patrick (21), ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho.
Kamanda Bwire amesema tukio hilo limetokea Juni 1, mwaka huu maeneo ya Kihesa.
Amesema siku ya tukio marehemu hakurudi nyumbani kwao jambo ambalo si kawaida yake, hivyo wazazi wake waliingiwa na hofu na kuanza kumtafuta.
“Marehemu alikuwa anaishi na wazazi wake, na huyu mtuhumiwa yeye alikuwa amepanga, Kwa hiyo siku ya tukio alitoka kwenda chuo, lakini mpaka usiku akawa hajarudi, ndipo wazazi walianza kupata wasiwasi, wakampigia simu rafiki yake lakini hawakufanikiwa,” amesema Kamanda Bwire.