
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo June 3 2021 Ikulu Dodoma amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame uliowasilishwa na Mjumbe Maalum na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda,Dkt. Vincent Biruta.

Katika ujumbe huo, Rais Kagame ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli , amempongeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa Rwanda ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.
Rais Kagame amesema hali ya Rwanda ni shwari na ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ukiwepo mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na ujenzi wa Reli ya kisasa ya kuunganisha Jiji la Kigali (Rwanda) na Isaka (Tanzania) ambayo itasaidia usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam kwenda Rwanda.
Rais Samia amemshukuru Kagame kwa kumtumia ujumbe huo uliojumuisha salamu za pole na pongezi na amemuhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda.


