×

Kaizer Chiefs Yakubalia Kuwaachia Mastaa

IMEFAHAMIKA kuwa Yanga ipo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Kaizer Chiefs, Lazarus Kambole kwa mkopo wa mwaka mmoja wa kukipiga Jangwani.

 

Yanga hadi hivi sasa tayari imefikia makubaliano mazuri na baadhi ya wachezaji kwa ajili ya kuichezea timu hiyo sambamba na kuwasajili wengine akiwemo Mkongomani Shaban Djuma wa AS Vita Wachezaji wanaotajwa hadi hivi sasa kuwepo mipango ya kusajiliwa na timu hiyo ni Denis Kibu wa Mbeya City, Daudi Bryson wa KMC, kipa Jeremia Kisubi anayekipiga Tanzania Prisons.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Chiefs imekubali kumtoa kwa mkopo wa mwaka mmoja baada ya kufikia muafaka mzuri kati ya klabu hizo mbili zenye mahusiano mazuri.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa dili hilo lilitarajiwa kumalizika leo (jana) baada ya viongozi wa klabu ya Chiefs kukutana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said huko Sauzi.

Aliongeza kuwa tofauti na dili hilo, pia watafanya mazungumzo ya kufanikisha usajili wa kiungo mkabaji raia wa nchini Kenya Anthony Akumu ambaye ana uwezo wa kucheza beki wa kati.

“Chiefs wamekataa kumuuza Kambole na badala yake wamekubali kumtoa kwa mkopo wa mwaka mmoja wa kuja kuichezea Yanga.

 

“Pia Akumu huenda akajiunga na Yanga kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja kama mazungumzo yatakwenda vizuri kati ya pande zote mbili Chiefs na Yanga.

 

“Hilo linawezekana kwetu kuwapata wachezaji hao wawili kutokana na mahusiano mazuri yaliyokuwepo kati yetu Yanga na Chiefs,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga Injinia Hersi Said, hivi karibuni aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa “Yanga tutasajili wachezaji wote waliokuwa katika mipango yetu na hakuna kitakachotushinda kwani tupo tayari kuvunja benki kwa kutumia gharama yoyote katika kufanikisha usajili.”

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave a Comment