
Kibongobongo mastaa wa kike kwa sasa ni wengi na karibia wote wanafanya vizuri. Hebu mtazame mtu kama Zuchu, Nandy, Anjela, Maua Sama, Lady Jaydee na wengineo. Wanajituma ile mbaya kuhakikisha wanafikisha ujumbe na kutoa burudani maridhawa kwenye jamii.
Lakini listi yote hiyo inaweza isikamilike bila kumtaja mwanamama kibotabo, Mwanaisha Nyange au Dayna Nyange.

Hivi karibuni Dayna ameshika vichwa vingi vya habari Afrika baada ya kuachia mkwaju mmoja matata akimshirikisha staa mkubwa wa muziki kutoka nchini Nigeria, David Adedeji Adeleke almaarufu Davido.
Ishu hii imewafanya baadhi ya watu wakiwemo mastaa wenzake kutoamini kisha kuishia kumpongeza kwa hatua kubwa aliyofikia.

Kama ilivyo desturi ya gazeti namba moja la mastaa nchini Tanzania la IJUMAA limekaa kitako na Dayna kwenye mahojiano maalum (exclusive interview) ambaye awali aliwahi kutamba na ngoma zake kama Komela, Nivute Kwako, Salama, Angejua na sasa ni Elo akiwa na Davido.
IJUMAA: Mambo vipi?
DAYNA: Poa, za siku nyingi…
IJUMAA: Salama kabisa, kwanza nianze kwa kukupa hongera kwa ngoma kali ya Elo uliyomshirikisha Davido…
DAYNA: Asante sana.
IJUMAA: Ulikutana vipi na Davido hadi mkafikia hatua ya kufanya kazi pamoja?
DAYNA: Unajua kuna kitu watu hawakijui, mimi na Davido hatujajuana leo wala jana, tulikuwa tukiwasiliana kwa kipindi kirefu kidogo, lakini maongezi yetu yalikuwa ni kuhusu mambo mengine tu na siyo kazi.
IJUMAA: Sasa ikawaje mpaka mkafanya kazi pamoja?
DAYNA: Kuna muda tu ulifika mimi na menejimenti yangu tukaona kuna kitu cha kufanya pamoja na Davido, basi tukazungumza naye na kupanga siku ya kuonana na kweli muda ulipofika tukaenda mpaka nyumbani kwake na kuzungumza naye jambo ambalo nataka kufanya naye.
IJUMAA: Baada ya kuzungumza naye ikawaje? Alikubali kirahisi tu?
DAYNA: Hapana, haikuwa rahisi sana kwa sababu baada ya kuongea naye, kwanza akaomba kusikiliza ngoma yangu na baada ya hapo akaipenda, basi ndiyo mwisho wa siku tukaingia studio.
IJUMAA: Vipi kuhusu malipo, yalikuwaje?
DAYNA: Mmmh! Kiukweli nisiwe muongo, siwezi kusema kuna malipo yoyote niliyompa Davido. Kifupi alichoangalia kwangu ni ubora tu wa kazi yangu ndiyo uliomvutia na siyo vinginevyo. Pia watu wanatakiwa watambue kwamba Davido ni msanii ambaye ana pesa nyingi sana hivyo sidhani kama kuna pesa yoyote ambayo ingemfaa kwa ajili ya kolabo na mimi.
IJUMAA: Unajisikiaje kuwa msanii wa kwanza wa kike kufanya kazi na Davido?
DAYNA: Najisikia vizuri sana na naamini hata Davido mwenyewe aliliona hilo ndiyo maana akaamua kuniheshimisha.
IJUMAA: Unahisi wasanii wengine wa kike wanakwama wapi kufanya kazi na mastaa wakubwa kama Davido?
DAYNA: Nadhani labda ni suala la muda tu kwa sababu kila mtu ana mipango yake katika kazi anayofanya. Mfano; kama mimi mipango yangu ni kuendelea kufanya kolabo na mastaa wakubwa duniani na ninaamini ipo siku nitafikia malengo.
IJUMAA: Umekaa Nigeria kwa kipindi kirefu na umekutana na wasanii mbalimbali akiwemo Davido, hebu tuambie kitu gani kikubwa ambacho umejifunza kutoka kwao.
IJUMAA: Licha ya kwamba umefanya kolabo na staa mkubwa kutoka Nigeria, lakini muitikio wa wasanii wenzako umekuwa mdogo tofauti na vile ambavyo tulitegemea, unahisi sababu kubwa ni nini?
Dayna: Siyo wote ambao hawajanisapoti, kuna mastaa ambao wamenisapoti sana na kuna watu wengine ambao wameniposti kwenye akaunti zao bila hata mimi mwenyewe kujua hivyo nawashukuru wote hata wale ambao hawakupata muda wa kunisapoti.
IJUMAA: Wananzengo wanaongea sana kuwa ooh, sawa, umefanikiwa kufanya kolabo na Davido, lakini mbona yeye mwenyewe hajaposti kuonesha sapoti?
DAYNA: Mimi nashangaa kwa nini watu wanaongea yote hayo, unajua Davido, kitendo tu kwanza cha kukubali kufanya kazi na mimi na tukaingia lokesheni kushuti ni jambo kubwa sana kwangu, hayo mengine ni ya ziada tu.
IJUMAA: Vipi lakini umejisikia vibaya kwa yeye kutoposti wimbo wenu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii?
DAYNA: Siwezi kujisikia vibaya hata kidogo, kwa sababu binafsi naona ni jambo la kawaida tu, heshima aliyonipa kufanya kazi pamoja naye ni kubwa sana kuliko kuniposti kwenye akaunti yake ya Instagram.
IJUMAA: Unahisi kwa nini wimbo wako haujafanya vizuri sana huko mjini YouTube?
DAYNA: Binafsi tageti yangu kubwa kwanza ilikuwa ni kuwafikia Watanzania wote hivyo lengo langu limekamilika, tayari nimetimiza ndoto yangu ya kufanya kazi na Davido. Kwa hiyo ishu ya YouTube kutofanya vizuri ni suala lingine, naamini huko mbeleni mambo yatakuwa mazuri kwa sababu wimbo bado unapatikana kwenye ‘platforms’ zote.
IJUMAA: Kuna tabia yoyote ambayo unaichukia kutoka kwa mastaa wenzako?
DAYNA: Zipo nyingi tu, lakini siwezi kuziongelea kwa sababu ni maisha ya mtu binafsi na uamuzi wake.
IJUMAA: Neno la mwisho kwa mashabiki wako, unawaambia nini?
DAYNA: Wimbo wa Elo bado upo YouTube, naomba waendelee kunisapoti na kuna vitu vingine vikubwa vinakuja.