×

Wasafirishaji Wamuanguakia Rais Samia Sheria ya Ubebaji Mizigo ya Zambia

WADAU wa usafirishaji katika bandari ya Dar es Salaam ukiwemo Uwakilishi wa Vyama vya usafirishaji na Chama cha Wakala wa Bandari wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya usafirishaji kwa wakati.

 

Mbali ya pongezi hizo, pia wameiomba Serikali kuingilia kati sheria inayopendekezwa nchini Zambia inayotaka asilimia 50 ya mizigo kutoka nchini ibebwe na raia wa nchi hiyo pekee, kwa kile walichokisema kuwa inaleta upinzani badala ya ushindani wa biashara kati ya Tanzania na Zambia.

Akizungumza leo Juni 24, 2021 jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukumay amesema wadau hao wanapongeza hatua ya Serikali kuboresha bandari hiyo ili iweze kubeba mizigo tani milioni 30 na spidi ambayo Rais Samia anakwenda nayo wanaamini hilo linawezekana.

 

Akifafanua kwa kina kuhusu sheria hiyo pendekezwa nchini Zambia,  Lukumay alisema, “Tunachokiona kwa wenzetu ni jambo ambalo linahitaji kutolewa ufafanuzi kidogo kwa sababu Wazambia wanataka kubadili mfumo wa kubeba mizigo ya Zambia katika bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na mzigo wa Zambia kuja Dar, wanasema mizigo ya Wazambia ambayo mingi ni mafuta na madini Copper, kwa asilimia 50 ibebebwe  na wao.

 

“Hii maana yake ni kwamba asilimi 50 ya mizigo hiyo ibebwe na raia wa Zambia, asilimia 30 ya mizigo ibebwe na TAZARA na asilimia 20 iliyobakia ibebwe na wengine… kumbukeni hapa nyumbani kuna wasafirishaji ambao wamekuwa kwenye biashara hiyo  kwa muda mrefu,” amesema.

Ameongeza wadau hao waliopo nchini wamekopa fedha na wamewekeza kwenye biashara hiyo.

“Leo tukifika hatua ya kugawana biashara hii kwa asilimia maana yake watanzania waliowekeza watafilisika na watakosa mizigo lakini Mungu aliyetupa bandari hii tutaona kama urembo, tutakuwa tunaona magari ya wenzetu tu yanapita.

“Sisi hatupingani na mtu yoyote anayetaka kufanya biashara kwa soko hurua, tuko tayari kushindana kwa ubora wa huduma na bei lakini hatuko tayari kuona tunashinda kwa watu kutumia sheria kukandamiza wengine, ndio maana tunaiomba Serikali iingilie kati suala hili.

 

“Na hii tunaisema kwa nia njema tukiamini sisi kama nchi hatuwezi kuruhusu utaratibu huo lakini pia hatutaki kuwanyima Wazambia stahili yao ya msingi ya kuja kuchukua mzigo, tunachosema tushindane kwa huduma na hizi huduma ndizo zitakazoamua nani atafanya zaidi lakini sio kutumia sheria,” amesema.

 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA), Elitunu Maramia amesema hatua ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kutatua changamoto za wadau wa usafirishaji ni muhimu na ina tija kwa taifa.

 

Amesema kwa sasa bandari inabeba takribani tani milioni 17 na kwa juhudi zinazofanywa kuna muelekeo wa kufikia tani milioni 30 siku zijazo.

Leave a Comment