
KOCHA wa viungo wa Simba, Adel Zrane amesema kuwa, ana uhakika kikosi chao kitapata matokeo ya ushindi katika michezo yote miwili wanayotarajiwa kucheza na wapinzani wao wa jadi, Yanga ndani ya mwezi ujao.
Simba na Yanga zinatarajia kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumamosi hii ambao ni wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, na baadaye kuvaana katika fainali ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa Julai 25, mwaka huu.

Jumamosi iliyopita, Simba walifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Songea.
Hii ni fainali ya pili mfululizo kwa Simba katika michuano hiyo baada ya msimu uliopita kucheza dhidi ya Namungo na kutwaa ubingwa.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha Zrane alisema: “Tumefurahi kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho, kwa kuwa hii ni hatua moja ya kukaribia zaidi katika kukamilisha malengo ya kutetea taji hili ambalo tulilipata msimu uliopita.
“Hii inamaanisha tutakuwa na michezo miwili ya dabi dhidi ya Yanga mwezi ujao, na naamini tutaibuka na ushindi katika michezo yote miwili.”