×

Nandy Atoboa Siri Kuachana Na Billnass

JINA kwenye kitambulisho cha Nida ni Faustina Charles Mfinanga. Ila wengi wanamtambua kama Nandy kutokana na kuwika kunako Bongo Fleva.

 

Kwa sasa ndiye msanii wa kike ambaye amefikia hatua ya kuandaa tamasha lake mwenyewe linalokwenda kwa jina la Nandy Festival na kujaza umati kwenye viwanja vikubwa vya mpira Bongo.

 

Nandy mwenye umri wa miaka 29, amezaliwa mkoani Kilimanjaro na kuanza kutumbuiza akiwa na umri mdogo wa miaka mitano tu.

 

Wakati huo alikuwa akiimba kwenye kwaya ya shule za Jumapili katika Kanisa la KKKT hadi pale alipokutana na Ema The Boy; prodyuza wa THT ambaye ndiye aliyempikia Wimbo wa Nagusagusa na kufanikiwa kugusa mioyo ya wengi.

 

Miongoni mwa nyimbo za Nandy zilizotamba na zinatamba hadi sasa ni pamoja na Aibu, Hazipo, Na Nusu, Nibakishie, Acha Lizame, Leo Leo, Number One, Kivuruge, Ninogeshe, Bugana, Nifundishe Wema na nyingine nyingi.

Kama kawaida; Gazeti la IJUMAA limekaa kitako na Nandy kwenye mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mambo mengi kuhusu maisha yake ya kimuziki na binafsi.

 

Kubwa ni ile simu aliyopigiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kunako stejini jijini Dodoma, wikiendi iliyopita na ishu nzima ya kuachana na mchumba’ke, William Lymo ‘Billnass’;

IJUMAA: Hongera kwa muendelezo wa Nandy Festival…

 

NANDY: Asante.

IJUMAA: Hivi karibuni wakati ukiwa kwenye mwendelezo wa shoo zako jijini Mwanza ulitamka hadharani kuwa upo ‘singo’, ulikuwa na maana gani?

NANDY: (anacheeeka) ile ni sehemu ya kuwapa burudani mashabiki wangu, ndiyo maana nikasema vile ili waburudike.

 

IJUMAA: Je, Billnass ambaye wengi wanajua ni mchumba’ko, aliposikia kauli yako unadhani alijisikiaje?NANDY: Sidhani kama atajisikia vibaya kwa sababu sijaongea kwa nia mbaya, halafu watu wamenitafsiri tu tofauti. Mimi nilikuwa namaanisha kuwa singo kwa namna nyingine, siyo kwa hiyo waliyoitafsiri wao.IJUMAA: Ulikuwa unamaanisha kuwa singo kwa namna gani?

 

NANDY: Kuna kuwa singo kwa namna nyingi, kwa hiyo watu waelewe hivyo, sikumaanisha kuwa nimeachana na Billnass.IJUMAA: Sasa mbona siku hizi hatuoni tena zile mbwembwe za picha mitandaoni kama ilivyokuwa zamani na kuna tetesi kwamba mmeachana?

 

NANDY: Mimi na Billnass ni watu wazima sasa, kwa hiyo kuna kipindi kinafika lazima tuweke maisha yetu siri, halafu tayari tulishafikia kwenye hatua kubwa ya uchumba, kwa hiyo tulishauriwa kuacha kabisa mambo ya mitandao ndiyo maana siku hizi hamuoni tena zile mbwembwe.

 

IJUMAA: Huoni kama mnawanyima mashabiki wenu haki yao?

 

NANDY: (anacheeeka) kivipi tena jamani, mimi naamini wanatupenda na kama mtu anakupenda kwa dhati, basi atakuwa tayari kukuona ukifanikiwa tu na siyo kuharibikiwa.

 

IJUMAA: Mashabiki walitegemea pia kumuona Billnass kwenye tamasha lako la Nandy Festival, lakini imekuwa tofauti, sababu ni nini hasa?

 

NANDY: Hakuna sababu kubwa, ila naomba mashabiki waendelee kufuatilia shoo zangu, ipo siku watamuona jukwaani.

 

IJUMAA: Umeshawahi kufikiria siku moja kumzalia Billnass?

 

NANDY: Kama Mungu akijaalia na mimi ni mwanamke, kuingia leba ni lazima.IJUMAA: Unahisi wasanii wengine wa kike wanakwama wapi kuandaa matamasha kama unavyofanya?

 

NANDY: Sijajua, lakini naamini kila mtu ana ndoto na malengo yake. Labda ipo siku nao wataandaa, ni suala la muda tu.

 

IJUMAA: Ulijisikiaje baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kukupigia simu ukiwa stejini jijini Dodoma?

 

NANDY: Ni jambo kubwa katika harakati ambazo ninazifanya kupitia Nandy Festival, nikiwa kama binti na yeye akiwa kama mama, imenitia nguvu kama mtoto kwa hiki ninachokifanya. Mama anaona kila hatua ambayo vijana wake tunapiga.IJUMAA: Kwa hatua hiyo uliyofikia, unamuahidi nini Mama Samia?

 

NANDY: Naahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa mfano kwa mabinti na vizazi vijavyo.IJUMAA: Aidia ya wimbo wako mpya wa New Couple uliitoa wapi?

 

NANDY: Ni aidia ambayo ilikuja tu na nikaamua kuimba kwa sababu kila siku watu wanapendana, halafu mwisho wa siku wanaachana. Ni ngoma ambayo inawagusa watu wengi na niliimba kwa hisia zote.

 

IJUMAA: Kuna tetesi kwamba umewahi kuwa kwenye Lebo ya WCB ya Diamond Platnuz, je, ni kweli?

 

NANDY: Ni kweli kuna kipindi ilikuwa nisajiliwe WCB, lakini kuna mambo yalitokea, kwa hiyo haikuwezekana tena hivyo nikaenda THT.

 

IJUMAA: Hivi lile bifu lako na Gigy Money liliishia wapi?Nandy: No comment (sina maoni).IJUMAA: Kuna tetesi kwamba ulikosana na Tanasha Donna, je, ni kweli?

NANDY: Mmmh! Hapana jamani! Mimi na Tanasha hatujawahi kukosana hata siku moja.

 

IJUMAA: Lakini inasemekana umemu-unfollow (kumuondoa kwenye wafuasi wako) kwenye Instagram, hii imekaaje?

NANDY: Hakuna kitu kama hicho.

IJUMAA: Ile kolabo yako na Tanasha imefikia wapi?

NANDY: Kolabo ipo palepale, muda ukifika kila kitu kitakuwa sawa.

 

IJUMAA: Unawaambia nini mashabiki wako?

 

NANDY: Waendelee kunisapoti, EP yangu ya Taste ipo YouTube, waendelee kuisikiliza na kutazama, watainjoi muziki mzuri.

Leave a Comment