BAADA ya kuvuna pointi tatu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameonekana mzuka umepanda akitaka kushinda mechi zote zilizosalia, hiyo ni baada ya kuwarudisha mzigoni wachezaji wake.
Yanga iliyofikisha pointi 70 baada ya kucheza michezo 32, ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, imesaliwa na mechi mbili dhidi ya Ihefu na Dodoma Jiji.
Mechi inayofuata ni Julai 14, mwaka huu ambapo Yanga itaikaribisha Ihefu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kisha Julai 18 itamaliza kazi ugenini dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema: “Wachezaji wetu leo (jana) wamerejea kambini baada ya kupewa likizo ya siku tatu ikiwa ni baada ya kufanya kazi kubwa ya kuibuka na ushindi mbele ya Simba.
“Wanaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na michezo unaofuata tukianza kucheza dhidi ya Ihefu, kisha Dodoma Jiji.“
Mpaka sasa kikosi kina majeruhi mmoja ambaye ni Balama Mapinduzi, wachezaji waliobaki wote wapo fiti kwa ajili ya kumalizia msimu kwa kushinda mechi zote.
”Yanga kwa sasa inahitaji pointi moja tu kujihakikishia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, kisha kujikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Stori na LEEN ESSAU,Dar es Salaam

