×

Hatma ya Uchaguzi TFF Julai 16

SAKATA la maombi ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeingia katika sura mpya ambapo sasa kesi hiyo imepelekwa mbele mpaka Julai 16, mwaka huu, uamuzi utatolewa.

 

Kesi hiyo imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais katika mchakato wa uchaguzi huo, Ally Saleh dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Wajumbe wa Bodi.

 

Jana kesi hiyo ilisomwa kwenye Mahakama Kuu ambapo Wakili Frank Chacha ambaye anasimama upande wa mlalamikaji, Ally Salehe, alisema: “Shauri dogo namba 305 linaomba zuio la harakati zote za uchaguzi kusimama mpaka kesi namba 98 ya mwaka 2021 itakaposikilizwa.

 

“Leo (jana) kesi imesikilizwa na upande wetu tumetoa hoja kwa nini uchaguzi usitishwe, na wenzetu wametoa hoja kwa nini uchaguzi uendelee. Baada ya kusikilizwa pande zote, kesi hii imeahirishwa mpaka Julai 16, mwaka huu kwa ajili ya kutolea maamuzi.”

 

Ikumbukwe kuwa, mara baada ya mchakato wa usaili kumalizika na rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia kubaki peke yake kwenye kuwania nafasi hiyo, ndipo ikafunguliwa kesi hiyo ya kuzuiwa kwa uchaguzi.

 

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Agosti 7, mwaka huu jijini Tanga, ambapo mbali ya nafasi ya urais, kuna nafasi sita za kamati ya utendaji zinawaniwa.

Stori: Denis Mtima,Dar es Salaam

Leave a Comment