Jeshi la Magereza Serikali imeanzisha Operesheni Maalumu ijulikanayo kwa jina la ‘Operesheni Punguza Mahabusu’ kwa lengo la kukabiliana wingi wa mahabusu na mzigo wa kuwahudumia katika magereza nchini.
Hayo yamesemwa jana Jumapili Julai 11 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza katika kikao kilichohusisha wafungwa na mahabusu wanawake katika gereza la Ruanda jijini Mbeya.
“Miongoni mwa mambo ambayo Rais Samia Suluhu Hassani hapendi kuyaona ni mrundikano na muongezeko wa watu katika magereza hasa wanawake, kwa kuwa anaamini wanawake ndio wanaojenga nchi na jamii wakishirikiana na wanaume.
“Kikubwa tunaichukua changamoto na tayari tunaanzisha operesheni maalumu itakayoitwa Operesheni punguza Mahabusu,” amesema Chilo.
Ameongeza pia kuwa, tayari serikali imeanza kuyaendea mbio baadhi ya mambo ikiwemo changamoto ya kuchelewa kwa upelelezi, utolewaji dhamana kwa kesi ndogo alizosema zinaongoza kwa kujaza mahabusu wengi katika magereza.
Akizungumzia hali ya msongamano katika gereza hilo Mkuu wa Gereza la Wanawake, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Rehema Mwailunga alikiri kuwepo kwa msongamano unaosababishwa na mkoa wa Mbeya kuwa na Mahakama ya kanda.
“Ili kupunguza msongamano, nashauri tuone umuhimu wa kujenga bweni la wafungwa na mahabusu wa kike sambamba na hili lililopo hapa,” alisema SSP Rehema.
Katika ziara hiyo, pia Naibu Waziri Chilo alitoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo magodoro, Taulo za Kike, Miswaki na sabuni kwa wafungwa na mahabusu hao.
