×

Mafuriko Ujerumani Yaua Zaidi ya Watu 21

Takribani watu 21 wamefariki dunia huku wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo, kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Magharibi mwa Ujerumani.

 

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi la Ujerumani, zinaeleza kwamba maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni katika Majimbo ya Rhineland- Palatinate na North Rhine-Westphalia, ambapo nyumba kadhaa na magari yamesombwa na mafuriko.

 

Mafuriko hayo ambayo pia yamezikumba nchi za Ubelgiji na Uholanzi, yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha barani Ulaya, na kusababisha kubomoka kwa kingo za mito kadhaa.

Meya wa Jimbo la Rhineland-Palatinate, Malu Dreyer ameyaita mafuriko hayo kuwa ni janga la kitaifa na kueleza kuwa vikosi vyote vya dharura, vimeelekeza nguvu zake kuwaokoa watu waliokwama kwenye mapaa ya nyumba zao pamoja na kuwatafuta wale ambao hawajulikani walipo kutokana na mafuriko hayo.

 

Inaelezwa kwamba zaidi ya watu 70 hawafahamiki walipo katika Wilaya ya Ahrweiler ambako kingo za Mto Ahr unaopeleka maji yake kwenye mto mkubwa wa Rhine, zilivunjika na kusababisha mafuriko ya kihistoria.

 

Helikopta za polisi na mamia ya maafisa wa jeshi la nchi hiyo, wametawanywa kwenye maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na mafuriko hayo, huku taarifa zikieleza kwamba kuna idadi kubwa ya watu waliokwama kwenye mapaa ya nyumba zao, wakisubiri kuokolewa.

Baadhi ya shule nchini humo zimefungwa kwa dharura huku miundombinu ya reli na barabara ikiathiriwa vibaya na mafuriko hayo.

 

Shirika la Utangazaji la SWR, linaeleza kwamba takribani nyumba 25 zipo kwenye hatari ya kubomoka kutokana na mafuriko hayo, katika Wilaya ya Schuld bei Adenau iliyopo katika Mkoa wa Eifel ambako hali ya dharura imetangazwa.

Leave a Comment