KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes ameibuka na kutamba kuwa walistahili kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na ubora wa wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo katika msimu huu.
Kati ya usajili bora uliofanywa na Simba ni Luis Miquissone, Larry Bwalya, Clatous Chama, Joash Onyango na Chris Mugalu ambao wamefanikisha ubingwa wa ligi msimu huu.
Simba tayari ni mabingwa wa ligi katika msimu ambao Jumapili hii watakabidhiwa kombe lao mara baada ya mchezo dhidi ya Namungo FC utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Jumapili.
Akizungumza na Championi Jumatano, Gomes alitoa pongezi nyingi kwa wachezaji wake ambao walitimiza majukumu ya uwanjani katika kupambana ili wapate matokeo kwa kuanzia ligi, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka huu.
Gomes alisema kuwa vijana wake walipambana katika mazingira tofauti wakiwa uwanjani, hivyo wanastahili pongezi pamoja na viongozi na wachezaji waliokuwa wanajitokeza uwanjani kuwasapoti.Aliongeza kuwa anajivunia ubora wa wachezaji wake wote waliojitoa uwanjani kufanikisha kupata matokeo mazuri ambao umewawezesha kubeba ubingwa huo wa ligi huku wakipanga kubeba Kombe la FA.
“Haikuwa kazi rahisi kwetu kuchukua ubingwa wa ligi, kiukweli tulistahili kubeba ubingwa huu kutokana na kuwa na kikosi bora kinachoundwa na wachezaji wenye ubora.
“Siku zote wachezaji ndiyo wanaipa matokeo mazuri na ili upate matokeo mazuri lazima uwe na wachezaji bora kama hawa niliowakuta Simba.“
Pia niwapongeze viongozi tuliofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa pamoja na mashabiki waliokuwa wanajitokeza uwanjani kutusapoti, tunakwenda kwenye fainali ya FA, hivyo niwatake wachezaji, viongozi na mashabiki kuungana kwa pamoja kwenda kupata matokeo mazuri ya ushindi yatakayotupa ubingwa,” alisema Gomes.
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam
