×

Breaking News: Mama Anna Mghwira Afariki Dunia

TAARIFA zilizotufikia hivi punde ni kwamba, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira amefariki dunia leo Alhamisi, Julai 22, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru, Arusha, ndugu wa familia wamethibitisha.

Mdogo wa Anna Mghwira na marafiki zake wa karibu wamethibitisha kutokea kwa kifo hicho leo.

 

“Ni kweli Mghwira amefariki mchana huu, alikuwa amezidiwa akawa amepelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU),” amesema mdogo wake.

 

Zaidi ya wiki moja iliyopita alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nkoaranga kwa tatizo la kupumua ambapo baadaye hali yake kuwa mbaya alihamishiwa hospitali ya Mount Meru.

 

Mwaka 2015, Dkt. Anna Mghwira aligombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha ACT Wazalendo ambapo aliibuka nafasi ya tatu huku mshindi akiwa Dkt. John Pombe Magufuli (CCM) na nafasi ya pili ilishikwa na Edward Lowassa (Chadema wakati huo).

 

Baada ya uchaguzi huo, Rais Magufuli alimteua Dkt. Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, cheo ambacho amekitumikia kwa takribani miaka sita hadi alipostaafu mwezi June, mwaka huu.

Leave a Comment