
ISHU hot mitandaoni kwa sasa inawahusu mapacha wawili wanaofanana kinoma, kuamua kwa hiyari yao kuolewa na mwanaume mmoja.
Mapacha hao Anna na Lucy DeCinque kutoka nchini Australia wamechumbiwa na mwanaume aitwaye Ben Byrne ambaye ni fundi umeme.
Wanawake hao ambao habari zao zimekuwa gumzo, mbali na kumzawadia ndoa mwanaume huyo wamepanga pia kumzalia watoto kwa wakati mmoja huku wakisisitiza kuwa wangependa watoto wao wasijue nani ni mama yao.
Anna anasema wamekuwa kwenye mazungumzo na familia zao kuona namna ambavyo wataweza kubeba ujauzito kwa wakati mmoja ili waweze kujifungua pia kwa wakati mmoja.
Anasema, anatamani kuona yeye na ndugu yake hakuna anayejivunia mwanaye bali watoto wao waweze kulelewa na mama wote wawili kwa mapenzi makubwa.
“Hakuna hata mmoja kati yetu anayefikiria kuwa na mtoto binafsi sote tunataka kuona huyu ni mtoto wangu na huyo ni mtoto wako”, alisema Anna huku Lucy akikubali, kwa kusema: “Tutashirikiana.”
Wanawake hao wameeleza namna ambayo wanaamini kuwa wao ni “mtu mmoja” hivyo wamekuwa wakivaa nguo sare na kula milo inayofanana na kwamba wamekuwa wakifanya yanayofanana kwa kila kitu.
Pamoja na uamuzi huo wa kuolewa na mwanaume mmoja kukubalika kwenye familia yao, baadhi ya ndugu wamepinga mpango wa kuwafanya watoto wao walelewe kwa ushirikiano kwa vile unaweza kuleta madhara kwa watoto hao.
Jamaa mmoja katika familia alisema, mtoto kuwa na mama yake kunaleta utulivu wa akili na hivyo kuendelea kushauri kuwa ni vyema kila mwanamke akalea wa kwake.
Hata hivyo, Anna alibaki kushikilia msimamo wake kwa kusema, angependa kwa vile baba wa watoto atakuwa mmoja ingekuwa heri watoto nao wafahamu kuwa wana mama mmoja.