×

AZANIA na NHIF Wazindua Huduma ya Ushirika Afya Kwa Wakulima Kupitia Mikopo

Mkurugenzi Mkuu wa Bendi ya Azania, Charles Itembe akizungumza kwenye mkutano huo.

 

 

Dar es Salaam: 3 Agosti, 2021: Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Benki ya AZANIA, leo wameingia makubaliano rasmi ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kunufaika na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya.

Mkurugenzi Mkuu NHIF Bw. Benard Konga

 

 

Katika makubaliano haya, Benki ya Azania itamlipia mkulima gharama ya bima ya afya kwa wakati na mkulima huyu atairejesha bila riba wakati wa msimu wa mavuno na mauzo ya mazao husika.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania kushoto na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga wakisainishana mkataba huo. Anayeshuhudia katikati yao ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege. Waliosimama nyuma yao ni maofisa wa taasisi hizo mbili.

 

 

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo, Mkurungenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe amesema Benki ya Azania iko mstari wa mbele katika kuhudumia kundi la wakulima kwa namna mbalimbali na sasa kwa makubaliano haya itamwezesha mkulima kujiunga na bima ya afya kwa kulipia michango kwa mwaka ili wakati wa msimu wa mavuno na mauzo ndipo airejeshe bila riba yoyote juu yake.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania, Charles Itembe na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga kulia wakibadilishana mikataba. Anayeshuhudia ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege.

 

 

“Tunaungana na Serikali yetu katika kuhakikisha wakulima nchini wanafanikiwa kwa kuwa na uhakika wa matibabu na katika hili Benki ya Azania tutamchangia mkulima mchango wa bima ya afya wa mwaka wa Shilingi 76,800 na mwenza wake kiwango hicho hicho na kwa kila mtoto Shilingi 50,400 kwa mwaka.

 

 

Kwa kuanzia tunakusudia kuwawezesha wakulima 2,000 kujiunga na Ushirika Afya, nia yetu ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watanzania wengi wanakuwa na bima ya afya kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza” alisema Bw. Itembe.

 

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bwana Bernard Konga amesema kuwa, ushirikiano huo na Benki ya Azania utawawezesha wakulima wa mazao mbalimbali nchini walio kwenye Vyama vya Ushirika kunufaika na huduma za matibabu kupitia bima ya afya bila kuwa na changamoto ya kifedha.

 

 

“Mfuko umeazimia kuwafikia watanzania wote na huduma za bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi kama ilivyo azma ya Serikali yetu ya kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya. Hii ndio maana tumekubaliana na Benki ya Azania ambao ni wadau wakubwa wa wakulima nchini kuwawezesha wakulima kujiunga na bima ya afya  bila changamoto ya kifedha” alisema Konga.

 

 

Akizungumzia huduma, Konga alisema kuwa mkulima na familia yake atapata huduma zote za matibabu katika mtandao mpana wa vituo zaidi ya 9,000 Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Rufaa ya Taifa.

 

 

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege akiongea katika tukio hilo, alipongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya Azania na NHIF katika kuwanufaisha wakulima na huduma za bima ya afya. Alionesha wazi kuwa mpango huu wa Ushirika Afya kwa wakulima una nafasi kubwa ya kuleta maendelea ya kilimo nchini kwani mkulima atakuwa na ujasiri wa kuendelea na kazi zake huku akiwa na uhakika wa matibabu wakati wowote atakapohitaji kwani ana kadi yake ya NHIF.

 

 

“Sote ni mashahidi, ugonjwa huja bila taarifa na mara nyingi magonjwa yamewaacha wakulima kwenye changamoto kwa sababu inawabidi watumie fedha yote waliyonayo na mara nyingine kukopa ili kujitibia au kumtibia mwanafamilia.

 

 

Kwa mpango huu unaoletwa na NHIF na Benki ya Azania, mkulima hana hofu juu ya huduma za matibabu wakati wowote yeye na familia yake” alisema Dk. Ndiege. Aliongeza kusema Vyama vya Ushirika tuko tayari kufanya kazi na Benki ya Azania na NHIF ili wanachama wake waweze kunufaika.

 

 

Pia alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kuchangamkia fursa hii na kuwaelimisha wanachama juu ya manufaa ya mpango huu wa Ushirika Afya kwenye vyama vyao vya ushirika popote walipo nchini.

Leave a Comment