×

Simanzi! Ndugu Wawili wa Familia Moja Wauawa na Polisi

MAELFU ya waombolezaji wamekusanyika katika uwanja wa shule ya msingi ya Kianjokoma kaunti ya Embu jana Ijumaa, Agosti 13, 2021 kutoa heshima za mwisho kwa kaka wawili waliodaiwa kuuawa na maafisa wa polisi Agosti 1, 2021.

 

Benson Njiru Ndwiga na Emmanuel Mutura walikutwa wameuawa ambapo miili yao ilikutwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Embu baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuvunja sheria za kafyu (masharti maalum yanayotolewa na rais). Spika wa bunge la Kenya, Justin Muturi alikuwa miongoni mwa waombolezaji na ametaka haki itendeke kwa familia ya marehemu.

 

“Ningependa tena kutuma pole zangu kwa familia kufuatia vifo vya wapendwa wao, tunapoendelea na uchunguzi na kutafuta haki, ningependa mashirika husika ya usalama kuhakikisha washukiwa wanakabiliwa vilivyo kisheria,” Muturi alisema.

Catherine Wawira, ambaye ni mama ya wavulana hao alisema hana la kusema kwani vifo vya wanawe vimeacha pengo kubwa moyoni mwake na ana huzuni mwingi sana. Wawira hangestahili kutizama majeneza ya watoto wake yalipofikishwa nyumbani kwake mapema hii leo kutoka mochuari kwa ajili ya mazishi.

Miili ya Benson na Emmauel ilifikishwa katika uwanja wa shule ya msingi ya Kianjokoma ikiwa kwenye magari mawili tofauti ya kubeba maiti. Marehemu wamepumzishwa jana nyumbani kwa wazazi wao eneo la Kithangari Kianjokoma Kusini mwa Embu.

 

Miili hiyo iliondolewa katika makafani ya hospitali ya Embu level 5 Ijumaa, Agosti 13 ambapo imekuwa ikihifadhiwa tangu siku ya Jumapili walipopoteza maisha yao. Aidha, viongozi wengine waliohudhuria mazishi ya wawili hao ni mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua na rais wa chama cha mawakili Nelson Havi.

Kulingana na Waziri Matiang’i uchunguzi unaendelea vema na ana matumaini kwamba chanzo cha vifo vya wawili hao kitabainika hivi karibuni. Uchunguzi wa awali wa vifo hivyo ulionyesha kwamba ndugu hao walifariki dunia kutokana na majereha waliopata vichwani na kwenye mbavu.

 

“Mashirika husika yanafanya uchunguzi, kitengo chetu cha usalama wa ndani kikishirikiana na shirika la IPOA kishaanzisha uchunguzi. Nimekutana na baba wa wavulana hao nikiwa na mwanasheria mkuu na inspekta jenerali wa polisi, tutafanya kila kitu kadri ya uwezo wetu ili haki itendeke kwa familia,” Matiang’i alisema.

Wengine waliohudhuria ni mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, mwenzake wa Mathira Rigathi Gachagua na rais wa chama cha mawakili nchini Nelson Havi. Hakuna afisa wa polisi hata mmoja aliyehudhuria mazishi hayo. Hii huenda ikawa kwa sababu mauaji ya wawili hao yamehusishwa pakuwa na polisi.

Ingawa uchunguzi wa maiti ulionyesha kwamba wawili hao walikuwa na majeraha yaliotokana na kupigwa silaha butu kichwani na kwenye mbavu, polisi wamesisitiza kwamba kaka hao waliruka kutoka kwenye gari lao lililokuwa likiendeshwa kwa kasi.

Leave a Comment