
ASKOFU Mkuu wa kanisa la Ufufuo na Uzima lenye Mako Makuu yake, Ubungo Maji jijini dar es Salaam ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kawe (CCM), Josephat Gwajima ameendelea na msimamo wake na waumini wake kuwa kutochanjwa chanjo ya corona huku awamu hii akisema kuwa Bunge likilazimisha, hatochanjwa.
Hata hivyo, ufafanuzi uliotolewa na Ofisi ya Bunge hivi karibuni umesema hakuna mbunge aliyelazimishwa kupata chanjo hiyo kwani chanjo ni hiari.
Akizungumza katika ibada yake jana Jumapili, Agosti 15, Askofu Gwajima alisema chanjo hiyo inayoendelea kutolewa nchini hazijafanyiwa utafiti wa kina kubaini madhara yake kwa wanaochanjwa na vizazi vijavyo.
“Wanaotaka nifukuzwe CCM watumie akili, kwa mfano tukichanja wote halafu kufikia 2025 watu wako hoi tutapigaje kampeni, bora wengine tubaki tusaidie kutetea chama chetu.
“Kulikuwa na twitter inasambaa kwamba wabunge wote wachanjwe, baadae Ofisi ya Bunge ikakanusha nikasema hata ingekuwa kweli mie nisingechanjwa, ni heri kurudi hapa nyumbani, ubunge ni mzuri una heshima unasaidia wananchi lakini kunichanja hapana,” amesema askofu Gwajima.
Hata hivyo amesema hapingi chanjo kwa ujumla wake: “Sipingi chanjo ila hii haijafanyiwa tafiti za kutosha kwa maana hiyo nasema hapa hachanjwi mtu. Mimi sio adui yenu nalinda kizazi chenu kijacho na Tanzania yetu ijayo kwa nguvu zangu zote.”