
RAIS wa Afghanistan, Ashraf Ghani ameikimbia nchi yake jana Jumapili, Agosti 15, 2021 jioni baada ya wanamgambo wa Taliban kuuzingira mji mkuu wa Kabul, kuingia Ikulu na kuchukua nchi.

Maafisa wawili wa serikali ambao hawakutaka majina yao kutajwa wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa Ghani ameondoka Afghanistan na inaarifiwa amekimbilia taifa jirani la Tajikistan.

Mkuu wa Baraza la Maridhiano ya Taifa nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah pia amethibitisha habari hizo kupitia mkanda wa video. Kuondoka kwa Ghani kunatoa taswira halisi ya uwezekano wa kundi la Taliban kuchukua madaraka nchini Afghanistan wakati wowote kuanzia sasa.

Wapiganaji wa kundi hilo waliingia kwenye viunga vya pembezoni mwa mji mkuu wa Kabul leo Alfajiri baada ya kupata mafanikio makubwa katika siku za karibuni kwa kuikamata miji mingi nchini humo.

Mwezi mmoja uliopita, Rais wa Marekani alisema bila kumung’unya maneno kuwa Taliban kuchukua nchi hakuwezekani kwa sababu jeshi la Afghanistan liko imara.