×

Bunge Kubadili Mchakato Viti Maalumu

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema wanatafuta namna bora ya kuwapata wabunge wa viti maalumu kwa wapigiwe kura na watu wote tofauti na sasa ambapo wanapigiwa kura na wajumbe.

 

Akifungua Kongamano la Walimu Wenye Ulemavu Tanzania jijini hapa jana, Spika Ndugai alisema wanafikiria kuwa na wawakilish wa moja kwa moja waliochaguliwa na wananchi na wasiwe viti maalumu wanaopigiwa kura na watu wachache.

 

“Ni vizuri wanawake wanaoingia bungeni wakichaguliwa na wananchi wenyewe moja kwa moja…. Lakini kwa namna gani hapo ndipo kuna mtihani; tukipata mfumo mzuri njia hiyo itakuwa ya kidemokrasia sana,” alisema.

 

Kuhusu walimu, Ndugai alisema ni watu muhimu katika jamii kutokana na mchango wao mkubwa katika elimu na malezi nchini.

 

“Bunge linasimama pamoja na walimu wa Tanzania katika kushughulikia maslahi yenu pamoja na hayo mnatakiwa kutimiza wajibu wenu vizuri kwani hakuna haki bila wajibu,” alisema.

 

Akizungumzia madhara ya virusi vya corona vinavyosababisha Covid-19, ndugai aliwahimiza walimu nchini wakiwamo wenye ulemavu kujitokeza kupata huduma za chanjo dhidi ya corona ili kujikinga dhidi ya maambukizi na madhara ya virusi vya corona.

 

Katibu Mkuu wa Chama wa Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema kongamano hilo limelenga kuchochea maendeleo ya walimu wenye ulemavu na kuchochea demokrasia.

Leave a Comment