×

Rais Samia: Unaweza Kukuta Gaidi Umepanga Naye Nyumba Moja – Video

Rais Samia Suluhu Hassan leo Agosti 25, 2021 anafungua kikao kazi cha siku tatu cha Maofisa Wakuu wa Makao Makuu, Makamanda wa Mikoa na Vikosi vya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.

 

“Ninawapongeza maofisa wakuu waandamizi, askari na watumishi wa jeshi la polisi ambao wataagwa Agosti 28 mwaka huu, kwa utumishi wao uliotukuta katika taifa letu. Kufikisha umri wa kustaafu bila kufukuzwa kazini si jambo dogo. Tutaendelea kutumia uzoefu wwenu.

 

“Wanaostaafu hawa naomba watoke na kibindo cha stahiki zao, tusizalishe tena madeni ya wastaafu Serikali ikabaki na mlolongo wa madeni. Kazi ifanywe kila anayetoka ajue stahiki zake anazipata wapi, waondoke wakiwa wamekamilika.

 

“Sote tunafahamu kwamba amani na usalama ndio msingi wa maendeleo katika nchi, Jeshi la Polisi mnalo jukumu kubwa sana kulinda amani yetu, bila amani hatuwezi kujenga uchumi wetu wala kuendesha shughuli za kisiasa.

 

“IGP Sirro amesema makosa ya uhalifu yamepungua kutoka 56,367 mwaka 2019/20 mpaka 49,508 mwaka 2020/2021. Tanzania makosa yanayotendwa yako kiwango cha chini.

 

“Kesi za usalama barabarani zimepungua karibu nusu, huenda hizi ni kesi zilizosajiliwa kwenye madaftari yenu, huenda kuna kesi haziji vituoni sababu watu wamekata tamaa, wakija hawapati haki zao, au vituo vya polisi vipo mbali, wanamalizana na kujichukulia sheria.

 

“Niwapongeze Jeshi la Polisi, nilipoingia watu walijaribu jaribu nikasema kama mliweza kule nyuma kwa nini msiweze leo. Kauli yangu mliifanyia kazi leo tunasikia Dar es Salaam iko kimya. Tunasikia mara moja moja mikoani, niwaombe wa mikoani kafanyeni kazi yenu.

 

“Fanyeni kila mnaloweza kufanya nchi hii ibaki salama, nchi hii iepukane na unyang’anyi na vitendo vya ujambazi. Naelewa mnafanya kazi katika mazingira magumu lakini naamini pamoja na changamoto mlizo nazo jitahidini kufanya kazi zenu.

 

“Naomba mkae na wadau wengine muangalie uwezekano wa kurekebisha sheria ya kumuweka mtu mahabusu. Kwenye nchi nyingine za wenzetu, mtu hakamatwi mpaka upelelezi ukamilike. Akikamatwa siku mbili, tatu, anawekwa ndani, wiki mahakamani, tayari anahukumiwa.

 

“Kwa zile kesi ambazo mnauhakika upelelezi hautakamilika, hao watu [mahabusu] watolewe wakafaidi uhuru wao wakiwa nje. Kwa zile kesi ambazo mnauhakika upelelezi utatimia, basi uharakishwe.

 

“Ni aibu kuona kwenye simu zetu tunarushiwa vi-clips askari wa jeshi la polisi ana negotiate [patana] na raia achukue rushwa hasa upande wa trafiki. Askari anachukua rushwa hana aibu, na hawajui kuwa mtu aliyemo ndani ya gari anamrekodi hata kwa kalamu.

 

“Kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu, IGP…hili nalo naomba mlitizame. Kesi za watu kufariki kwenye vituo vya polisi haipendezi machoni kwa watu, inaichafua serikali na tendeni yaliyo haki.

 

“Dunia sasa ipo katika wimbi la nne la mapinduzi ya viwanda linaloongozwa na mifumo ya TEHAMA, Jeshi la Polisi ni sehemu ya sekta zinazofanya kazi duniani, lazima tujipange katika eneo hilo. Mfumo wa TEHAMA una faida nyingi na changamoto nyingi zikiwemo za mtandao.

 

“Nataka polisi mrekebishe sheria ya kuweka mtu mahabusu, nchi nyingine mtu hakamatwi hadi upelelezi ukamalike, serikali inabeba mzigo wa maelfu ya mahabusu wakati upelelezi haujakamilika, naomba muangalie hayo ili mtoe huduma zinazofaa kwa watu wetu

 

“Kuhusu kesi za kubambikizwa, nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kuweka ukomo wa upelelezi kufikia miezi 6 kwa kesi ndogo. Mpaka 22 Agosti 2021, idadi ya mahabusu jela ni karibu sawa na wafungwa. Hadi juzi wafungwa walikuwa 16,542 wakati mahabusu 15,194.

 

“Mlivamia bucha mkachukua nyama za watu, walipolalamika mkasema tumefanya vile kwa sheria, lakini ukiangalia kwa undani kilichotendeka hakuna sheria hapo. Naomba mliangalie hilo na mengine, tuko hapa kuhudumia watu, siyo kudidimiza watu.

 

“Kutokana na mawimbi ya kuenea kwa ugaidi, magaidi sasa wana technique ya kukaa ndani ya raia huko mitaani wanajichanganya. Yawezekana umepanga naye nyumba moja lakini humjui huyu ndiye. Jeshi la Polisi tujenge urafiki na raia, wawe na moyo wa kutuambia nani ni nani,” amesema Rais Samia.

 

Leave a Comment