
RAFIKI, ukiwa na mtu mpende kwa dhati hadi aone kweli wewe unamaanisha kumpenda, siyo vinginevyo.
Kumpenda mtu kwa dhati, kunasaidia kumfanya ajione wa maana katika maisha na hiyo inasaidia kuondoa kasoro mbalimbali zikiwamo za kufanya ngono nje ya ndoa.
Ukweli ni kwamba, ikiwa kweli unataka maisha mazuri ya ndoa ni lazima kujifunza namna ya kupendana kwa dhati na kuacha unafiki kama walivyo baadhi ya watu.
Msingi wa maisha yanayofaa ni kuona kama mnaendana. Ukiona kama hamuendani, siyo sahihi kuulazimisha moyo.Hili nalisema hasa kwa wale ambao bado hawajaoana.
Kwa walio kwenye ndoa, kama kunatokea kutoelewana, cha msingi ni kuzungumza, kwa sababu kuachana ni jambo baya, linalosumbua hata watoto na kuharibu mfumo wa maisha kwa jumla.
Tunaishi katika ulimwengu, ambao makosa ni mengi. Kwa maana hiyo, siyo sahihi hata kidogo kufikiria kuachana mnapokuwa na mtu, badala yake angalia namna gani mnaweza kwenda sawa.
Mkipendana na kuoneshanahuruma kwenye uhusiano au ndoa, ndipo mtakapoishi na kupata faraja.Kila mtu anaweza kujibu swali hilo kadri anavyotaka. Wengine wake zao ni wafanyakazi wa ndani, hawana mamlaka ya kuuliza kuhusu biashara wala kipato; hii siyo sahihi.
Kwa wapenzi, kutopendana au kutohurumiana huwa ndiyo msingi wa kuharibika kwa kila kitu katika maisha yao. Ndiyo kusema, ni jambo muhimu zaidi kwa kila mtu aliye katika uhusiano, kufikiria mbinu za kufanya, ili kumpenda zaidi mwenzi wake.Lakini kwa sasa kwa kweli hali siyo ya kufurahisha sana.
Kuna nyumba nyingine, mwanamke akiwa mja mzito, hapo ni tiketi ya mwanaume kwenda nje ya ndoa na kuanza kudharau familia.Kuna wanaume wengine kwa sababu yeye ni mwanaume, hata kama mke anaumwa vipi, hayuko tayari kusaidia hata kupika au kuchota maji.
Hii siyo sawa hata kidogo. Wengine ndiyo kwanza anaondoka kabisa nyumbani. Upendo ni kusaidiana na kuhurumiana.
Yeyote ambaye anaishi kwa jeuri na mkewe au mumewe, ajue kwamba anajitafutia mikosi mwenyewe katika maisha yake. Ni vigumu kufanikiwa, wakati watoto wanalia labda wameshindwa kupelekwa shule nzuri au wanaishi kwa shida, eti baba anahangaika na wanawake wengine nje ya ndoa.
Kwa sasa kama unafanya haya, huwezi kujua ninachokieleza. Lakini muda unakuja, utapata majuto dhahiri ya yale mabaya unayowafanyia watoto na familia yako kwa jumla.
Kuna mambo mengi ya kufanya, ili muendelee kuyafurahia mapenzi yenu, baadhi yake ni kwamba unatakiwa ujue hisia zake ziko wapi, yaani anapenda hasa vitu gani?Kama ndivyo, unapaswa kujenga uaminifu juu yake na wewe mwenyewe kuwa mwaminifu hadi mwisho. Hicho ndicho kitakachowasaidia kuwa imara katika mapenzi yenu.
Kwa sababu mko mbali, hamuwezi kuonyeshana hisia zenu za jinsi gani mnapendana ana kwa ana, njia pekee ya kuonyeshana hisia zenu ni mawasiliano ya mara kwa mara.
Hii ni pamoja na kutumiana ujumbe mfupi wa simu, barua pepe au kuwasiliana kwa njia nyingine zozote za mawasiliano ya kompyuta.
Lakini pia ni suala la msingi kuonyesha unajali pale mwenzi wako anapowasiliana nawe. Jitahidi kuwasiliana naye kadri anavyowasiliana nawe.
Katika maisha ya mapenzi ni vizuri kujitahidi kujibu kila unapoitwa au kuulizwa. Kuna wengine wana dharau, wanajifanya wako bize, wakati siyo kweli.Wengine unaweza kuwaona wako bize na simu wakati mwenzi wake anamuuliza jambo fulani, jambo ambalo siyo sahihi hata kidogo.
Hakikisha unatimiza ahadi zako kwamba jitahidi kufanya na kutimiza yale uliyoahidi utafanya na epuka kuahidi ukijua huwezi kutimiza ahadi yako.Tafakari, chukua hatua kwani watu wanaingia kwenye mapenzi siyo kwa sababu wanataka karaha, bali raha.Unaweza kumdharau mpenzi wako, lakini kumbuka hiyo ni hatari. Anaweza kukuletea Ukimwi na mambo mengine, ambayo hukuyategemea.Katika maisha, jitahidi kuwa na hekima, jitahidi kumfanyia wema mwenzi wako!Kwa leo naishia hapa, tukutane IJUMAA ijayo.