×

Mbowe na Wenzake Wasomewa Mashtaka Upya

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu wasomewa upya mashtaka yao sita mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

 

Mbowe na wenzake wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Ijumaa Septemba 10, 2021 ambapo kwa mara ya kwanza Leo wataruhusiwa na Mahakama hiyo kujibu tuhuma zinazowakabili kwa kusema ndio wanakubaliana na tuhuma au hapana hawakubaliana na tuhuma hizo.

 

Mbowe anashtakiwa pamoja na Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya ambao wote ni makomandoo waliofukuzwa kazi jeshini kutokana na sababu mbalimbali.

 

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo ya awali namna wanavyodaiwa kutenda makosa yao na wakili wa Serikali, Tulimanywa Majingo. Baada ya kusomewa maelezo hayo washtakiwa wamekubali taarifa zao binafsi na wamekana mashtaka yote.

 

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa wamesomewa idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka ambao ni 24 na vielelezo zaidi ya 19.

 

Kwa upande wa utetezi, Wakili Peter Kibatala amesema wanatarajia kuwa na mashahidi 11, wakiwemo washtakiwa wenyewe, huku mashahidi wanne Kati ya hao, akiomba Mahakama asiwataje majina yao na anuani zao kwa sababu za kiusalama.

 

Kutokana na hali hiyo, Jaji Mustapha Siyani ameahirisha kesi kwa muda ili apitie vifungu vya sheria kabla ya kuja kutoa uamuzi.

 

Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka jana.

 

Vilevile wanatuhumiwa kupanga vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko na kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

 

Leave a Comment