×

Sakho ni Balaa, Apiga Bao Lingine Simba

WINGA Msenegali wa Simba, Pape Osmane Sakho anazidi kudhihirisha ubora wake katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi baada ya kufunga bao pekee kwenye mchezo wa kirafiki hivi karibuni.

Simba wakiwa Arusha katika maandalizi ya msimu mpya na siku ya Simba Day walijikuta wakipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate FC.

Simba hawajapoteza mchezo wowote kuanzia wameanza maandalizi yao na nyota njema inaonekana kumwakia zaidi Sakho ambaye ameshashuka nyavuni mara tatu hadi sasa.

Katika michezo minne ya kirafiki, Sakho ambaye anatajwa kuwa mridhi wa Clatous Chama ameshafunga mabao matatu huku akisifiwa mara kwa mara na makocha wa timu hiyo.

Sakho ambaye amekuwa akifunga mabao safi ya kideoni, alifunga bao lake la kwanza katika mechi ya kirafiki Simba dhidi ya As Far Rabat Nchini Morocco, bao la pili alifunga kwenye mchezo dhidi ya Olympique Clud de Khouribda ya nchini Morocco huku akifunga la tatu jana dhidi ya Fountain Gate fc inayoshiriki Championship.

Huyu anaonekana kuwa atawasumbua sana TP Mazembe kwenye mchezo wa Simba Day, utakaopigwa Jumapili ijayo kwenye Dimba la Mkapa.

Hii itakuwa nafasi ya mashabiki wa Simba kwenda kuitazama timu yao mpya ambayo ina mastaa wakubwa kibao.

RICHARD PALLANGYO(SJMC), Dar es Salaam

Leave a Comment