×

TRA Yazindua Mnada wa Forodha kwa Njia ya Mtandao – Video

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua mnada wa forodha kwa njia ya mtandao ambapo sasa minada yote ya TRA, itakuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao tofauti na ilivyokuwa ikifanyika awali kwa njia za kawaida.

 

Kwa mujibu wa Afisa Msimamizi wa Kodi wa TRA, Julieth Kidemi wakati akizungumza na Kituo cha Redio cha +255 Global Radio kuipitia kipindi cha Front Page, TRA imeamua kuja na mpango wa minada kwa njia ya mtandao (Customs Online Auctions) kwa mizigo iliyopitisha muda ambayo imehifadhiwa katika maeneo ya forodha.

Maeneo hayo ya forodha ni pamoja na bandari, viwanja vya ndege na mipakani ikiwemo maeneo mengine ambayo bidhaa hizo huwasili na kuhifadhiwa zikisubiri kukamilika kwa taratibu za forodha.

 

Tofauti na mfumo wa awali, minada kwa njia ya mtandao, utarahisisha watu wengi zaidi kushiriki kwenye minada mbalimbali inayoendeshwa na mamlaka hiyo ambapo ili mtu ashiriki, atatakiwa kuwa na kifaa chochote kama simu, laptop au kompyuta yenye intaneti.

“Pia ili ashiriki, lazima awe na namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) ambayo hutolewa bure na mamlaka hiyo pamoja na anuani ya barua pepe (email adress) pamoja na namba ya simu uliyoitumia kusajilia TIN.

 

“Baada ya hapo, mtu anayetaka kushiriki kwenye mnada, ataingia kwenye tovuti ya TRA ambayo ni www.tra.go.tz na kujisajili kwenye kipengele cha Auction ambapo utatakiwa kuingiza taarifa zako kwa kifupi kisha moja kwa moja utakuwa na uwezo wa kushiriki minada yote inayoendeshwa na TRA mahali popote ulipo,” amesema Kidemi.

 

Afisa Msimamizi wa Kodi wa TRA, Julieth Kidemi akifafanua jambo katika Kipindi cha Front Page kupitia Global Radio mapema leo.

 

Ameendelea kueleza kuwa mamlaka hiyo imeamua kuendesha minada yake kwa njia ya mtandao na kuachana na utaratibu uliokuwa unatumika awali kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo kuhakikisha TRA inaondokana na changamoto zilizokuwa jitokeza kwenye minada ya kawaida.

 

Sababu nyingine ni kutekeleza Mpango Mkakati wa Tano wa TRA ambao unataka minada ya forodha ifanyike kwa njia ya mtandao, kutekeleza mpango Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwa na serikali mtandao ambapo wizara, idara, wakala na taasisi za serikali zinatakiwa kuendesha shughuli zake hasa za ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.

 

Sababu nyingine ni kukomboa kodi ya serikali kwa wakati kwa mizigo iliyoingia nchini na iliyokamatwa kwa sababu ya kutolipiwa kodi iliyopo katika maeneo ya forodha.

Akizungumzia faida za mfumo huu mpya wa kuendesha minada kwa njia ya mtandao, Kidemi amesema kwa utaratibu huu, bidhaa nyingi zinauzwa kwa wingi na kwa wakati na kwa ushindani ulio wa haki na hatimaye makusanyo ya kodi yanaongezeka.

 

Faida nyingine ni Watanzania wengi wenye nia ya kununua bidhaa kupata fursa ya kununua popote walipo bila kuongeza gharama kwa kutumia madalali ambapo pia wanunuzi wanakuwa na muda wa kutosha wa kununua bidhaa na kutakuwa na ushindani wa haki.

Pia mnunuzi ana uwezo wa kushindana kwa bidhaa zaidi ya moja kwenye mnada husika na mfumo huo umeunganishwa na mfumo wa Usajili wa Magari kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa kadi za usajili kwa washindi watakaonunua magari.

 

Kidemi ameongeza kuwa endapo mtu yeyote anayetaka kushiriki kwenye minada hiyo atakuwa na swali lolote au kuhitaji ufafanuzi, asisite kupiga simu katika Kituo cha Huduma kwa Mlipakodi kwa namba za bure ambazo ni 0800 750 075 au 0800 780 078. Pia, anaweza kutuma ujumbe kwa njia ya WhatsApp kwa namba 0744 233 333 au kutuma barua pepe kwenda: [email protected].

Leave a Comment