
HATIMAYE mwili wa mtoto Talia Essau Moshi mwenye umri wa miaka minne ambaye anadaiwa kuuawa kutokana na kupigwa na msichana wa kazi za ndani (House Girl) katika Kata ya Moshono jijini Arusha, umeagwa leo Jumanne, Septemba 21, 2021 na kusafirishwa kuelekea Marangu Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.
Msichana huyo wa kazi mwenye umri wa miaka 13 ambae tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na uchunguzi zaidi kufuatia tukio hilo la kunyama.
Mama wa marehemu aitwaye Janeth Temba amesema alipigiwa simu na msichana huyo na kuambiwa mtoto anaumwa ambapo alipofika nyumbani alimkuta mtoto ameshafariki huku majibu ya Hospitali baadae yakieleza kwamba chanzo cha kifo ni mtoto kupigwa na kuachiwa majeraha mbalimbali hasa kichwani.

“Nilipigiwa simu na msichana wa kazi akaniambia mtoto wangu anaumwa, anaharisha…. nikamuuliza sasa hivi anaendeleaje? Akaniambia nimempa dawa amelala, nikamwambia akiamka unipe niongee nae.
“Lakini zikapita kama dakika 10 akanipigia tena, akaniambia dada leo usichelewe amezidiwa, ndio nikawahi kuja huku nikakuta mtoto wangu tayari ameshafariki na amekua wa baridi.
“Majirani wakampeleka Hospitali ile kukaguliwa wakaambiwa ana majeraha yaliyovimbia damu kuanzia kichwani, mwilini wakasema ndio kitu kilichosababisha kifo chake,” asema Janeth Temba.