×

Morisson, CAS Yaibuka Mengine

UONGOZI wa Yanga, umeweka wazi kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imesogeza tena mbele hukumu yake dhidi ya aliyekuwa mchezaji wao, Mghana, Bernard Morrison kutoka Septemba 29 hadi Oktoba 21, mwaka huu.

 

Yanga ilikataa rufaa ya mchezaji huyo katika mahakama hiyo kubwa baada ya kushindwa kukubaliana na maamuzi na Kamati ya Maadili ya TFF ambayo ilimuidhinisha mchezaji huyo kujiunga na Simba wakati Yanga wakiendelea kudai bado wana mkataba naye.

 

Kwa mujibu wa mwanasheria wa Yanga, Alex Mgongolwa, CAS imeleta taarifa nyingine juu ya hukumu ya shauri hilo kwenda hadi Oktoba 21 kutoka Septemba 29, waliyoitangaza awali.

 

Mgongolwa alisema taarifa waliyotumiwa haijaeleza sababu ya kusogezwa mbele kwa kesi hiyo lakini kutokana na uzoefu wake, anaamini shauri la rufaa na madai kawaida huchukua muda mrefu kwa kuwa huonekana lina hoja ya msingi.

 

“Tumepokea taarifa ya kusogezwa mbele kwa hukumu ya shauri letu lakini haijaelezwa sababu za kupelekwa mbele ingawa siku zote shauri la rufaa au madai huchukua muda mrefu kutolea maamuzi kutokana na kuonekana aliyeleta madai kuwa ana hoja ya msingi.

 

“Taarifa waliyoileta ni kwamba Oktoba 26, mwaka huu ndiyo tarehe inayotazamiwa, alichokisema kwenye taarifa hiyo ni kwamba mwamuzi ameamua kupeleka mbele shauri la Yanga dhidi ya Morrison hadi Oktoba 26, tumewaambia kwamba tupo tayari kwa uamuzi wowote utakaotolewa,” alisema Mgongolwa katika mahojiano yake.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Leave a Comment