
MOTO uliozuka chini ya ardhi, kando ya Mto Uwashi, kijiji cha Momwe, wilayani Rombo na kuzua taharuki kwa wananchi imebainika kwamba chanzo chake ni mboji iliyokaa kwa miaka mingi na si mlipuko wa volkano kama ilivyodhaniwa awali.
Mkuu wa wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Hamisi Maiga aliliambia gazeti hili kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na wataalamu wa ardhi na maliasili wilayani humo umebaini chanzo cha moto huo kuwa ni mboji iliyorundikana chini ya ardhi kwa miaka mingi.
“Timu yetu ya wataalamu wa ardhi ilifika katika eneo la tukio ili kufanya uchunguzi wa awali nini chanzo cha moto ule, walichimba kwenye tabaka la kwanza la ardhi na la pili ila cha kushangaza chini kulikuwa hamna moto na hata mawe yalikuwa hayajaungua. Wakabaini kulikuwa na mbolea aina ya mboji iliyokaa miaka mingi.
Wanaamini ndio chanzo cha moto,” alisema. Aidha alisema pamoja na kubaini chanzo cha moto huo bado timu ya wataalamu wa jiolojia wanasubiriwa ili kufanya uchunguzi wa uhakika na kuwataka wananchi waondoe hofu.
Mtaalamu wa masuala ya ardhi na maliasili, Arbogast Mhumba alisema anaamini chanzo cha moto huo si volkano kwani volkano ikitaka kulipuka kunakuwa na dalili nyingi ikiwemo mawe kuyeyuka, kupasuka kwa miamba na kuwepo kwa njia.