×

Kimeumana! Mondi, Harmo, Barna Boy, Wizkid & Davido

WAANDAAJI wa Tuzo za All Music Award (AFRIMA 2021), Septemba 23, mwaka huu, wametaja listi ya majina ya wasanii, Ma-DJ, maprodyuza na waongozaji wa video (madairekta) kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

 

Tanzania imeng’ara kwa wasanii wake kutokea katika vipengele vingi vinavyowaniwa; Diamond Platnumz, King Kiba, Harmonize, Zuchu, Rayvanny, DJ Sinyorita, Darassa, Nandy, Director Kenny, Rosa Ree na Producer Lizzer, jumla ni 11.

 

Kutoka Nigeria wametokea wasanii kibao kwenye vipengele mbalimbali. Wamo Burna Boy, Davido, Wizkid, Olamide, Guchi, Zinoleesky, Rexxie, Tiwa Savage, Omah Lay, Zltan na wengineo.

 

Mchuano unaoneka kuwa mkali, kwani katika kila kipengele ambacho Mtanzania yupo, basi kuna Mnigeria hivyo hapatoshi!

 

Kama ni mfuatiliaji, basi unakumbuka kipindi ambacho muziki wa Tanzania ulivyokuwa ukipambanishwa na ule wa Afrika Kusini, lakini sasa upepo umebadilika, vita imeamia Nigeria.

 

IJUMAA WIKIENDA linakuja na uchambuzi mzito;

KIPENZI CHA MASHABIKI AFRIKA

Hapa kuna wasanii 10 wanaowania huku Mtanzania akiwa ni King Kiba pekee wakati Nigeria kukiwa na vichwa Vinne; Zinoleesky, Buju, Fire boy DML na Guchi.

 

Hakuna asiyeujua uwezo wa Fire Boy ambaye ametikisa katika soko la muziki duniani; kichwa kutoka Nigeria.

Fire Boy amewahi kuchaguliwa kwenye tuzo kubwa duniani na nyingine akaibuka mshindi. Kwa mwaka 2019, alichaguliwa katika tuzo mbili kubwa katika vipengele tofauti; The Headlines Award na City People Music Award.

 

Mwaka wa 2020, alijizolea tuzo zote katika vipengele vinne katika Tuzo za Headlies Award ambapo alichukua vipengele vya: Albam Bora ya Pop, Albam Bora ya RnB, Mwimbaji Bora wa RnB na Mwanamuziki Mhamasishaji.

Guchi naye siyo haba, anakimbiza kwa sasa, huku Zinoleesky na Buju nao wakiwa hawakamatiki.

 

Tanzania inawakilishwa na King Kiba, bila shaka hakuna wasiwasi naye kwani uwezo wake unajulikana. Mwaka 2016, Kiba alinyakua tuzo zote katika vipengele alivyochaguliwa katika Tuzo ya Watsup Music na BEFFTA kupitia wimbo wake wa Aje.

 

Mwaka huohuo alishinda tuzo mfululizo kama; ASAFA, Soundcity, TZ INSTA, Best Celebrity Player na WANNA MUSIC.

Mwaka 2019, akichomoka na ushindi katika vipengele viwili; Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki na Msanii Bora Mwonekano katika Video katika Tuzo za AFRIMA.

 

MSANII BORA WA MWAKA

Hiki ndicho kipengele kikubwa ambacho wengi wanakisubiria. Tanzania inawakilishwa na Diamond huku kukiwa na Wanigeria wanne; Burna Boy, Davido, Wizkid na Omah Lay na vichwa vingine kutoka nchi tofauti.

 

Simba hana kazi ndogo, kwani amekuwa gumzo zaidi duniani kutokana na uwezo wake. Kwani, licha ya kunyakua tuzo kubwa duniani pia amekuwa akivunja rekodi zilizowekwa na wasanii wakubwa Afrika kama Davido na Burna Boy.

 

Kupitia wimbo wake wa Waah, amevunja rekodi iliyowekwa na staa wa Nigeria, Davido ambapo Wimbo wa Waah ukiwa umefikisha watazamaji zaidi ya milioni 1 kwa saa 8 pekee huku Davido akifikisha watazamaji kama hao kwa saa 9.

 

Simba ameshachukua tuzo mbalimbali kama; WatsUp TV Africa Music Video, Channel O Music Video, HiPipo Music, Top Ten Tube Music, The Headies, The Future Music, Nzumari, MTV Europe Music, MTV Music, BET, African Muziki Magazine (ARIMMA), Tanzania Music, People’s Choice na na AFRIMA.

 

Kwa upande wake, Burna Boy anaitolea macho tuzo hiyo pia. Amekuwa msanii bora kwa miaka ya hivi karibuni huku akishinda tuzo kubwa duniani ambazo nyingine aliburuza Simba.

 

Kwa mwaka huu, Burna Boy alimpiga za uso Diamond ambaye walichaguliwa kuwania katika kipengele kimoja cha Msanii Bora wa Kimataifa katika BET Awards.

 

Pia kwenye kabati lake kuna Grammy Awards ambazo alichaguliwa mara mbili mfululizo; mwaka 2020 alishinda kupitia kipengele cha Albam Bora ya Dunia na albam yake ya Twice as Tall huku mwaka 2019, akifanikiwa kuchaguliwa katika kipengele cha Albam Bora kupitia albam yake ya The African Giant.

 

Wakati, hofu ikiwa juu ya Burna Boy, lakini pia hofu inaongezeka ambapo Wizkid, Davido na Omah Lay, wote kutoa Nigeria wanapochuana kuwania kipengele hicho. Ushindani ni wa kutisha mno.

 

KOLABO BORA AFRIKA

Vita inazidi kuwa nzito, kwani Watanzania wawili; Diamond na Nandy wamechaguliwa kuwania kipengele hicho huku Wanigeria nao wakiwa wamo wa kutosha tu; Bella Shmurda, Wizkid na Ladipoe.

 

Nandy anafanya poa mno Bongo huku akijaribu kuota mbawa na kutikisa hadi nje ya ya Bongo. Uwezo wake siyo wa kutilia shaka, kwani amefanikiwa kupata mashabiki wengi kupitia kazi zake anazozifanya.

 

Nandy amewahi kushinda Tuzo za AFRIMA mara mbili mfululizo mwaka 2017 na 2020. Nandy alitwaa tuzo hiyo kama; Mwanamuziki Bora wa Kike Ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Pia mwaka 2018, Nandy alishinda Tuzo ya AMI Award Afrika katika Kipengele cha Mwanamuziki Chipukizi wa Kike. Nandy anawania Kipengele cha Kolabo Bora Afrika kupitia wimbo wake wa Number One akiwa na Joeboy wa Nigeria.

 

Pia hali ni tete kwani Diamond naye anawania katika kipengele hichohicho kupitia wimbo wake wa Waah akiwa Koffi Olomide kutoka Kongo.

 

Wakati huohuo, Wizkid naye ametajwa kuwania katika kipengele hichohicho kupitia wimbo wake wa Essence akiwa na Terms wa hukohuko Nigeria. Ikumbukwe, Justine Biber alitokea kuupenda wimbo huo na kuomba kuufanya remix.

 

VIDEO BORA AFRIKA

Kazi zinazofanywa na waongozaji wa video za wasanii (directors) ni kubwa mno na siyo ya kubezwa. Katika kipengele hiki kuna washiriki 6 huku Director Kenny akiwa ni Mtanzania pekee, lakini kuna Wanigeria watatu; Dammy Twitch, Prior Gold na Unlimited LA.

Kenny amewahi kushinda Tuzo ya AFRIMA.

 

WIMBO BORA WA MWAKA

Katika kipenegele hiki kuna washiriki 11 ambapo wawili ni kutoka Tanzania, watano wakitoka Nigeria na wengine nchi mbalimbali.

Diamond; kupitia wimbo wake wa Waah na Rayvanny na wimbo wake wa Number One ndiyo wawakilishi wa Tanzania.

 

Nigeria wanawakilishwa na Davido na wimbo wake wa FEM, Wizkid na wimbo wake wa Essence, Patoranking na wimbo wake wa Abule na Olamide na wimbo wake wa Infinity. Mchuano ni mkali kwani wote wanowania katika kipengele hiki wana uwezo mkubwa.

 

MTAYARISHAJI BORA WA MWAKA

Katika kipengele hiki kuna Wanigeria wanne huku kukiwa na Mtanzania mmoja pekee, Lizzer. Laizer anaingia kwa kupitia wimbo alioutayarisha wa Waah ambao unafanya poa. Pia Laizer mkono wake wa dhahabu umetumika kutengeneza nyimbo kibao ndani za Wasafi na nje ambazo zimefanya poa.

 

Maprodyuza wa Nigeria nao wanazidi kuwapa Watanzania tumbo joto, kwani wote wanne, waliochaguliwa wana uwezo mkubwa. Npji ametayarisha Wimbo wa FEM, Telz ametayarisha Wimbo wa Abule huku P Prime akiwa ameutayarisha wimbo unaoitwa Infinity.

 

MSANII CHIPUKIZI ALIYEFANIKIWA

Katika kipengele hiki kuna wasanii kumi huku Mtanzani akiwa Zuchu pekee kupitia wimbo wake wa Sukari. Upande wa Nigeria kuna wasanii watatu; Bella Shmurda kupitia wimbo wake wa Cash App, Omah Lay kupitia wimbo wake wa Godly na Tems kupitia wimbo wake wa Damages.

 

MWANAMUZIKI BORA WA HIPHOP

Bongo tunawakilishwa na bidada Rosa Ree kupitia wimbo wake wa Satan. Upande wa Nigeria, kuna wasanii kama; A-Q kupitia wimbo wake wa Breath, Blaqbonez kupitia wimbo wake wa Bling na Vector kupitia wimbo wake wa Early Momo.

 

DJ BORA AFRIKA

Katika kipengele hiki kuna ma-DJ kumi huku Mtanzania akiwa mmoja, DJ Sinyorita. Upande wa Nigeria kuna Ma- DJ wawili ambao wanawania katika kipengele hicho hivyo ushindani si wa kitoto.

STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR

Leave a Comment