
THE Return Of Champions ndio kauli mbiu ya Yanga msimu huu katika kuhakikisha wanakusanya vikombe vyote ambavyo watashiriki msimu huu ukiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Bara kama ambavyo viongozi wa timu hiyo wamesema.
Leo Jumatano, Yanga wataanza kibarua rasmi cha kuutafuta ubingwa huo ambapo watavaana na Kagera Sugar, ugenini katika Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera.
Kuelekea katika mchezo huo, uongozi wa Yanga chini ya Mtendaji Mkuu, Senzo Mbatha, ameliambia Championi Jumatano kuwa, malengo yao ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono katika mchezo huo wa kwanza dhidi ya Kagera ili safari yao ya ubingwa ianze kwa kishindo huku wakiweka wazi kuwa kila mchezo ambao wataucheza msimu huu kwao ni kama fainali.
“Tuanaenda kucheza na Kagera Sugar ambayo ni timu nzuri na yenye mzoefu mkubwa na ligi kuu, tunakumbuka msimu uliopita walitusumbua pindi tulipokutana nao lakini tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo wetu wa kwanza ili safari yetu ya ubingwa iweze kuanza vyema.
“Malengo yetu msimu huu ni kuweza kuwa mabingwa wa ligi kuu ambapo klabu hii imeshindwa kuupata kwa misimu minne hivyo ili tuweze kufanikiwa katika hilo lazima tupigane katika kila mchezo na tucheze kama fainali, naamini tutafanikiwa,” alisema kiongozi huyo.
WATANO OUT YANGA
Aidha kuelekea katika mchezo huo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kuwa watawakosa wachezaji wao watano ambao ni Yassin Mustafa, Balama Mapinduzi, Saido Ntibazonkiza, Mukoko Tonombe na Dickson Ambundo.
“Katika mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar tutawakosa wachezaji wetu watano ambao ni Yassin Mustapha, Balama Mapinduzi na Saido Ntibazonkiza, ambao hawapo fiti huku Dickson Ambundo yeye akiwa ni majeruhi na Mukoko Tonombe bado akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo dhidi ya Simba katika fainali ya kombe la Shirikisho la Azam,” alisema kiongozi huyo.
Tangu msimu wa 2010/11, timu hizi zimekutana mara 22 ambapo Yanga imeshinda mara 17 na Kagera mara nne.
MATOKEO YAO YALIYOPITA
LIGI KUU BARA 2020/2021
Yanga 3:3 Kagera Sugar
Kagera Sugar 0:1 Yanga
LIGI KUU BARA 2019/2020
Kagera Sugar 0:1 Yanga
Yanga 0:3 Kagera Sugar
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam