
KATIBU Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, leo Alhamisi Septemba 30, 2021, amekutana na kuzungumza na washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika wa Shindano la Urembo na Utanashati Afrika 2021 kwa viziwi (Miss and Mr. Deaf Africa 2021) waliotoka nchi mbalimbali za Afrika walipotembelea moja ya johari za Tanzania; Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Shindano hilo linafanyika Tanzania kesho Oktoba Mosi, 2021, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi ya Afrika kuwa mwenyeji wa shindano hilo mashuhuri zaidi katika mabara mengine duniani.