×

Yanga Yawaondoa Mastaa Wake Dar

OFISA Mtendaji Mkuu wa mpito wa Yanga, Senzo Mazingisa, ameweka wazi kuwa ili kutimiza lengo lao la kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara unaotetewa na Simba, uongozi wa timu hiyo umekusudia kuvunja likizo ya muda mfupi kupisha michuano ya kimataifa, na kuwapeleka kambini wachezaji wa timu hiyo ili kujifua zaidi.

 

Yanga juzi Jumamosi waliendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

 

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi sita ambazo kabla ya michezo ya jana zilikuwa zinawaweka katika nafasi ya pili ya msimamo baada ya kucheza mechi mbili, wakizidiwa idadi ya mabao tu dhidi ya vinara Polisi Tanzania.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, mara baada ya ushindi wao dhidi ya Geita Gold, Senzo alisema: “Kwanza tumefurahi baada ya kufanikiwa kupata ushindi mwingine muhimu dhidi ya Geita Gold, ulikuwa mchezo mgumu lakini wachezaji wetu walipambana sana.

 

“Baada ya mechi hii tunajua kutakuwa na likizo fupi ya kupisha michezo ya kimataifa, lakini sisi kama uongozi wa Yanga tumekusudia kufuta mapumziko kwa wachezaji wetu na tunapanga kuwa na kambi ya muda mfupi ikiwezekana nje ya Dar es Salaam ili kujiweka sawa zaidi.

 

“Kama ambavyo tumeweka wazi kuwa msimu huu tunahitaji kushinda kombe la Ligi Kuu Bara hivyo, ni lazima tuwe na kikosi imara cha kufanikisha hilo na hii ndiyo sababu ya kuja na wazo la kuondoa likizo ili tuendelee na mazoezi.”

 

Hata hivyo, imefahamika kuwa Yanga wanakwenda kuweka kambi yao mkoani Arusha sehemu ambapo Simba waliweka kabla msimu huu haujaanza.

Leave a Comment