
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi amezipokea ndege mpya 2 za Serikali aina ya Airbus A220-300 kutoka nchini Canada. Tukio hilo limefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume visiwani Zanzibar leo Oktoba 8.
“Hadi sasa, Shirika letu la ndege limefikisha idadi ya ndege 11, kati yake zikiwemo Bombadiers, Dreamliner, na Airbus, lengo ni kuwezesha ATCL kuwa na ndege 16 ifikapo mwaka 2023. Mipango ya kuzipata ndege hizo inaendelea. Nawahimiza wananchi na wafanyabiashara kuendelea kutumia ndege zetu kwa huduma za usafiri.
“Sekta ya usafirishaji wa anga, majini na nchi kavu, ni msingi muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu na Mataifa yote duniani. Sekta ya usafirishaji ndio msingi mkubwa katika kukuza sekta za utalii, biashara, viwanda, kilimo, na shughuli za watu.
“Ni habari njema kuona kwamba, mkataba wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato Dodoma umesainiwa. Hivi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendeleza mazungumzo na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kukiimarisha zaidi kiwanja cha ndege cha Pemba.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,inaendelea kulikaribisha Shirika la ndege la Tanzania, Air Tanzania
ATCL katika kuimarisha usafiri wa Anga na sekta ya utalii.
“Sekta ya Usafiri wa Anga imeathirika sana,kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, ambao umeathiri sana sekta ya utalii na biashara. Haya ni mafanikio makubwa, tukijua kwamba,Sekta ya usafiri wa Anga, Majini na nchi kavu,ni msingi muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu,” amesema Rais Mwinyi.