
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amewahimiza wawekezaji wa Benki ya watu wa China kuhamasisha uwekezaji wa nje kwa wateja wa Nchini Tanzania.
Amezungumza hayo katika sherehe za maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja zilizofanyika jijini Dar es salaam katika makao makuu ya Benki ya DASHENG.
“Nimeona mahesabu na niseme wazi katika kipindi cha miaka miwili mliyokaa hapa nchini mmeweza kupata faida kubwa kwa kipindi cha mwaka huu mpaka hapo mwezi wa tisa tu pekee mmefikisha zaidi ya Bilioni tano faida, ni wazi mnaweza kufanya makubwa zaidi ya haya na kupitia serikali
ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan tutaendelea kuwaunga mkono wawekezaji wote wenye nia njema kama nyinyi, ila tunaomba sana mtushike mkono kupitia mtandao wenu wa biashara hebu tusaidieni watu wetu wapate fursa za kuwekeza nje ya nchi, hii itasaidia sana kupanua wigo mpana
wa uwekezaji wa kimataifa hapa nchini na ni faida kwa nchi zote mbili”, alisema mkuu wa Mkoa Amos Makala.
Aidha Bwana Makala amewataka wajasiriamali na wawekezaji wakubwa kutumia benki ya DASHENG kwani ni fursa nzuri sana ya kibiashara kwa Benki hii inayokua kwa kasi kubwa.
“Napenda kuwapongeza sana watu wa China kwa kuona umuhimu wa kufungua Benki hii ya DASHENG hapa Tanzania, nasisitiza sana watu kutumia fursa kama hizi kuwekeza, wajasiriamali wadogo waje kuomba mikopo katika Benki hii inayoingiza faida kubwa, na sisi kama serikali tunaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na wawekezaji kama hawa ambao wanalenga kuchochea mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yetu ya Tanzania.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa alisisitiza umuhimu wa sekta za fedha kutambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo ambao katika siku za hivi karibuni wamekua wakitanua soko lao kwa kasi kubwa.
“Napenda kusisitiza taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya DASHENG kuwa na mipango Madhubuti ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, muweke mipango wezeshi itakayowasaidia ikiwemo mikopo nafuu, kwa benki hii ambayo inaweza kutengeneza faida mapaka bilioni tano kwa kipindi kifupi, mtoe sehemu ya asilimia ya fedha hizo kuwapa watu mikopo, na nyinyi watu msisite kuja kuwekeza na kukopa Benki ya DASHENG ni ya kila mtu.
Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa amesema juhudi za serikali katika kuhamasisha uwekezaji zinaendelea huku akiamini kuwa kwa kufanya hivyo basi ni kutengeneza mazingira bora ya Biashara kwa wananchi lakini pia itasaidia serikali kuongeza pato la Taifa.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Benki ya DASHENG Guydon Chihwalo, amesema Benki ya DASHENG mpaka sasa tangu kuanzishwa kwake miaka miwili iliyopita ina uwezo wa kukopesha mpaka kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 23.
“Tunawasisitiza Watanzania kuja kuwekeza na sisi, tuna uwezo wa kukopesha mpaka Shilingi Bilioni 23 ni fedha nyingi hizi, nipende kuwaatarifu wateja wetu kwamba mizania yetu kwasasa inainyesha tumefikia Bilioni 112, na pia mpaka kufikia Septemba mwaka huu tumeweza kupata faida bila makato Bilioni 5, tunaweza kuwahudmia wateja wote wa nje ya nchi na ndani ya nchi”, alisema Guydon