×

Sabaya Alia na Vyombo vya Habari

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha leo Oktoba 28, 2021, imeendelea kusikiliza kesi namba 27/2021 ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita ambapo mawakili wa utetezi, wamewasilisha ombi mahakamani hapo, wakilalamikia gazeti moja la kila siku kuwa linapotosha taarifa kuhusu kesi hiyo.

 

Kesi ilianza kusikilizwa majira ya saa 10:30 asubuhi mbele ya Hakimu Mwandamizi, Dkt. Patricia Kisinda ambapo wakili wa serikali, Afmed Mtenga alisimama na kuieleza  mahakama kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kusikilizwa.

 

Kabla ya shahidi kuendelea, wakili upande wa utetezi anayemtetea Sabaya, Moses Mauna alisimama na kuomba kusajili malalamiko yao mahakamani hapo na kusema kuwa hoja yao ipo katika namna ambavyo kesi hiyo inaripotiwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti moja la kila siku.

 

Akaieleza mahakama kwamba kupitia ukurasa wa Instagram wa gazeti hilo, iliripotiwa habari kwamba cheti kilicholetwa na shahidi mahakamani hapo jana, Agosti 27, 2021 kilionesha Sabaya na wenzake wakiwa benki, jambo ambalo amesema siyo la kweli.

 

Mauna akaendelea kwa kueleza kwamba hii siyo mara ya kwanza kwa gazeti hilo kuripoti kimakosa habari kuhusu kesi hiyo, na kueleza kuwa Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) alipoitwa siku za nyuma mahakamani hapo kutoa ushahidi, gazeti hilo lilitoka na habari kubwa iliyosomeka ‘Meneja wa TRA Amkana Sabaya Mahakamani’, jambo ambalo alisema halikuwa na ukweli.

 

Akaongeza kuwa vitendo vinavyofanywa na gazeti hilo, havina madhara kwa upande wa utetezi pekee bali vina athari kwa upande wa Jamhuri na Mahakama kwa jumla ambapo hukumu itakapotolewa, watu wanaweza kuelewa tofauti kutokana na mambo waliyoaminishwa.

 

Akaiomba mahakama kupitia kifungu cha sheria namba 392 A cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, waandishi wa gazeti hilo pamoja na mitandao yake ya kijamii, wazuiwe kuripoti mwenendo wa kesi hiyo.

 

Baada ya wakili wa Sabaya kuwasilisha hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Ofmed Mtenga alisimama na kueleza kuwa ombi hilo litaathiri mwenendo wa kesi na kwamba mambo yanayolalamikiwa yamefanyika nje ya mahakama na hayajaathiri mwenendo mzima wa kesi hiyo.

 

Mabishano ya hoja kati ya mawakili wa utetezi na wa jamhuri yaliendelea, wakivutana kuhusu namna ombi hilo lilivyowasilishwa mahakamani hapo bila wahusika kutoka gazeti hilo kupewa taarifa zozote na kutakiwa kujieleza na mwisho, hakimu aliomba muda wa kwenda kuandika maamuzi ya mahakama juu ya ombi hilo.

Leave a Comment