
MWANAMKE mmoja mjamzito amefariki dunia katika ajali ya kuogofya karibu na Hospitali ya Virgin kwenye barabara ya Kenol-Murang’a kaunti ya Murang’a nchini Kenya wakati akiwa njiani kuelekea katika hospitali ya Maragua Level Four kujifungua
Akithibitisha tukio hilo, Mkuu wa Polisi wa Murang’a Kusini, Alexander Shikondi alisema ajali hiyo iliyotokea Jumatano, Novemba 3 ilihusisha magari mawili na pikipiki na kwamba Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Shikondi aliongeza kuwa mwanamke huyo mjamzito alikimbizwa katika Hospitali ya Virgin ambako baadaye ilibainika kuwa amefariki. Madaktari katika kituo hicho cha afya walisema mtoto huyo ambaye alikuwa tumboni pia aliaga dunia.
Watu wawili walionusurika ajali hiyo walipata majeraha mabaya na kulazwa hospitalini huku wengine wanne wakipata majeraha madogo.
Mama wa marehemu alisimulia alivyowasiliana na binti yake kwa njia ya simu muda mfupi kabla ya kufikwa na umauti. “Aliniambia anaumwa, nikamwambia aende hospitalini na kwamba nitamuona asubuhi. Muda mfupi baadaye nikapigiwa simu kuhusu ajali hiyo,” alisema mama huyo.