×

Rais Mwinyi Akutana na Sanjay Dutt Ikulu Zanzibar

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo Novemba 9, 2021 ameupongeza ujio pamoja na azma ya Muigizaji Nyota wa Filamu za Kihindi, Sanjay Dutt ya kutaka kuwekeza sambamba na kuwa Balozi wa kuitangaza Zanzibar kiutalii.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Muigizaji Nyota huyo wa Filamu za Kihindi, Sanjay Dutt  ambaye amekuja kuitembelea Zanzibar na kueleza jinsi alivyovutiwa na vivutio mbalimbali vilivyopo Unguja na Pemba.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi pia, alimpongeza Nyota huyo kwa kueleza lengo lake la kuanzisha Kampuni yake hapa Zanzibar ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha tasnia ya Filamu hapa nchini sambamba na kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii Kimataifa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba azma ya nguli huyo ya kuwekeza Zanzibar katika sekta za maendeleo zikiwemo Afya, Elimu na nyinginezo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane la kuwarahisishia wananchi kupata huduma muhimu.

Leave a Comment