×

Tanzia: Rais FW de Klerk Afariki Dunia

 

 

Rais wa zamani wa Afrika Kusini na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Amani, F.W de Klerk amefariki dunia asubuhi ya leo, Novemba 11, 2021 kwa kile ambacho familia imeeleza kwamba ni saratani ya ini iliyokuwa ikimsumbua kwa muda mrefu.

De Klerk alikuwa rais wa mwisho wa kitawala wa kikaburu nchini Afrika Kusini ambapo alitawala kuanzia mwaka 1989 hadi Mei, 1994 alipokabidhi madaraka kwa Waafrika Kusini weusi ambapo kwa mara ya uchaguzi wa kidemokrasia ulifanyika na kumuingiza madarakani Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo baada ya uhuru kamili.

Katika utawala wa Mandela, de Klerk aliteuliwa kuwa makamu wa pili wa rais na anatajwa kuwa miongoni mwa makaburu wachache waliosimamia kwa karibu mchakato wa kubadilisha utawala nchini Afrika Kusini utawala wa kibaguzi kwenda kwenye utawala wa kidemokrasia.

Taarifa za kifo cha de Klerk zimethibitishwa na msemaji wa Mfuko wa FW de Klerk Foundation, Dave Steward na kueleza kwamba amefikwa na mauti akiwa nyumbani kwake, Fresnaye akiwa na umri wa miaka 85 huku akiacha mjane, Elita, watoto wawili, Susan na Jan na wajukuu kadhaa.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusu kifo hicho ikiwa ni pamoja na kutoa taratibu za mazishi ya kiserikali.

Taarifa iliyotolewa Juni 8, 2021 na msemaji wa mfuko huo, ilieleza kwamba de Klark aligundulika kuwa na saratani ya kuta za mapafu ambayo kitaalamu hujulikana kama mesothelioma na mpaka anafikwa na mauti alikuwa akiendelea na matibabu.

De Klerk atakumbukwa na Waafrika Kusini wengi kwani ndiye aliyeagiza kutolewa gerezani Hayati Nelson Mandela bila masharti yoyote na kuruhusu siasa za kidemokrasia nchini humo na kuviruhusu vyama vya wazawa kama ANC, SACP, PAC na vingine vingi kuanza kujishughulisha na siasa kihalali.

Mwaka 1993, de Klerk na Mandela walitunukiwa kwa pamoja Tuzo ya Nobel ya Amani kwa jinsi walivyofanikiwa kubadilisha utawala nchini humo, kutoka ule wa kikaburu uliokuwa ukiwanyanyasa weusi mpaka kufikia utawala wa Kidemokrasia uliomuzesha Mandela kushinda nafasi ya urais mwaka 1994.

De Klerk alistaafu kwenye siasa za nchi hiyo mwaka 1997 na kutoa hotuba iliyowagusa wengi, akiomba radhi kwa niaba ya wenzake kwa madhila yote waliyoyapata Waafrika Kusini weusi katika kipindi chote cha ubaguzi wa rangi nchini humo.

 

Leave a Comment