×

Hakuna Aliyeweka Rekodi ya Harmo Bongo

HARMONIZE au Konde Boy Mjeshi kwa sasa anajiita Teacher (Mwalimu) kunako Bongo Flevani.

Hii ni baada ya kuachia albam yake mpya yenye jina la High School.

High School ni albam ya pili ya Harmonize ambayo imesheheni ngoma ishirini huku ikiwa imeshirikisha wasanii wa Tanzania kama Ibraah, Anjella pamoja na Sholo Mwamba.

 

Alabam hiyo pia imeshirikisha wasanii kutoke nje ya Tanzania kama Busiswa (Afrika Kusini), Eddy Kenzo (Uganda) pamoja na Sarkodie (Ghana).

Kati ya ngoma ishirini ndani ya albam hiyo ni ngoma moja tu ya Teacher ambayo tayari ilikuwa imeshatoka huku ngoma nyingine kama vile Influencer, Sorry, Outside, Always, Turn Up na nyinginezo zikiwa ni ngoma mpya kabisa ambazo kabla ya Ijumaa iliyopita zilikuwa hazijawahi kusikika.

 

Albam ya High School imesheheni ngoma ambazo zina vionjo tofautitofauti kwani kwenye ngoma kama Sandakalawe Remix na Teacher ameimba Amapiano na kwenye ngoma kama Muziki na Kamaliza ameimba Singeli.

Ngoma nyingine za kwenye albam hiyo ina vionjo vya Afro-Pop na Bongo Fleva.

 

Albam hiyo iliingia kwenye mitandao ya kusikiliza na kutazama muziki ikiwa ni saa chache baada ya Harmonize kufanya listening party kupitia akaunti yake ya Instagram.

Konde Boy ameeleza kuwa kuna baadhi ya ngoma kwenye albam hiyo zinahusu maisha yake binafsi.

 

Kwa mujibu wa Harmonize, Ngoma ya Sorry ni maalum kwa ajili ya mke wake wa zamani aliyetengana naye, Sarah Michelotti; raia wa Italia.

Ikumbukwe hii ni albam ya pili kutoka kwa Harmonize ambayo inakuja miezi ishirini baada ya ya albam yake nyingine ya Afro East ambayo ilikuwa ni albam yake ya kwanza; hakuna msanii aliyeweka rekodi kama hiyo kwenye Bongo Fleva; imewekwa na Harmonize pekee.

 

Kwenye albam hiyo ya bosi huyo wa Lebo ya Konde Music Worldwide kuna mambo kumi (10) unayopaswa kuyajua kama mdau au shabiki wa muziki wa Bongo Fleva;

Ni albam ya pili kutoka kwa Harmonize baada ya Afro East iliyotoka Machi 15, 2020; ikiwa na ngoma 18 alizowashirikisha wasanii kutoka ndani na nje ya Bongo kama Kenya, Nigeria na Jamaika.

 

Ni albam ya kwanza kutoka chini ya lebo yake ya Konde Gang Music. Afro East ilitoka akiwa bado hajaizindua Konde Gang na kabla ya hapo pia alikuwa ameachia EP yake ya kwanza ya Afro Bongo iliyotoka akiwa chini ya WCB Wasafi.

Ni albam iliyoshirikisha msanii mmoja pekee wa kike ambaye ni Anjella kutoka Lebo ya Konde Gang Music; hii ni tofauti na ile ya Afro East ambapo Lady Jaydee na Yemila Alade walisikika.

 

Katika albam hiyo, wasanii walioshirikishwa ni sita pekee ambao ni Anjella, Ibraah na Sholo Mwamba, wote kutoka Tanzania; wengine ni Sarkodie (Ghana), Naira Marley (Nigeria) na Busiswa (Afrika Kusini).

Ndani ya albam hiyo ni ngoma mbili pekee ambazo zimeshatoka zilizojumuishwa kwenye albam hiyo, nazo ni Sandakalawe na Teacher, hizo 18 zilizobaki ni mpya kutoka kwenye maganda yake.

 

Kwenye albam hiyo kuna ngoma moja yenye mahadhi ya Singeli inayokwenda kwa jina la Kamaliza ambayo amemshirikisha Sholo Mwamba. Pia kwenye Afro East kulikuwa na ngoma ya Singeli pia iliyokwenda kwa jina la Hujanikomoa.

Ndani ya lebo hiyo, wasanii wa lebo yake aliyowashirikisha ni Angella na Ibraah pekee; wengine kama Country Boy, Young Skales, Cheed na Killy hawajapata nafasi.

 

Harmonize hajashirikishwa msanii yeyote kutoka nchi nyingine za Afrika Mashariki zaidi ya Tanzania, wakati kwenye Afro East kuliko Khaligraph Jones wa Kenya aliwakilisha vilivyo.

Hadi kukamilika kwake, albam hii imepita kwenye mikono ya maprodyuza 12, kwa pamoja ndiyo wamekamilisha hizo ngoma 20 ikiwa ni wastani wa ngoma 1.66 kwa kila prodyuza.

 

Kwenye albam hiyo ya High School, Harmonize hajashirikisha msanii yeyote kutoka nje ya Bara la Afrika, lakini ikumbukwe kwenye Albam ya Afro East kulikuwa na kundi la muziki wa Rege kutoka Jamaika la Morgan Heritage.

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO

Leave a Comment