
MKURUGENZI wa Lebo ya Kondegang, Harmonize ameamua kuvunja ukimya na kuzungumza kwa mara ya kwanza kuhusu bosi wake wa zamani Diamond Platnumz na tofauti zao.
Harmonize amezungumza mambo mengi baada ya kurejea nchini akitokea Marekani huku akianika namna ambavyo aliingia kwenye bifu na Diamond kwa kile alichokieleza kuwa alichukuliwa kama anashindana nae.
Harmonize amefunguka alivyolipishwa mamilioni kuvunja mkataba na WCB huku akisema kuwa alijitahidi kuomba msaada kwa watu mbalimbali ili wazungumze na Diamond wayamalize kwa amani lakini Diamond hakuwa tayari.
“Lengo langu ilikuwa ni kutafuta peace, mimi nilikuwa naamini jinsi uwekezaji unavyokuwa mkubwa na mafaniko yatakuwa makubwa, Konde Gang ilikuwa ni ndoto yangu lakini sikutegemea kuifanya hivi karibuni.
“Kulikuwa hakuna jinsi lazima niondoke (WCB), nilichofanya, ni kujiuliza mtu gani ambaye angeweza kuzungumza na bro, nikaona Boss Joe (Joseph Kusaga), alikuwa mshkaji wake wakati huo wanataka kufungua media.
“Nikamfuata na kumueleza ukweli kuwa kuna hiki na hiki, sikumficha. Kusaga akaniambia ataongea nae lakini akakausha, nikasema hapa hakuna kinachoendelea.
“Nikamwambia Boss Kusaga, akasema nimuonyeshe mkataba wangu, nikamuonyesha akasema mkataba huo una vitu vingi na hata akinitafutia mwanasheria siwezi kulipa fedha. Nikamwambia sitaki anitafute mwanasheria, kuna mambo mawili, aongee na bro tukayamalize au au nitafute njia ya kulipa fedha za kuvunja mkataba.
“Ninachotaka mimi ni amani, akasema atanirudia, ila hakunirudia, nikasema hapa nimekosa msaada. Nikamfuata mama yake Nasibu, mama Dangote, nikamueleza kuwa kuna vitu siridhiki navyo.
“Tumetoka mbali na bro, sikutaka kuondoka vibaya, nilitaka nimfanye yeye awe nguli wa muziki Afrika, afeel proud kunisainisha mimi. Mi niko straight, ukinichukia sawa, usitake leo nikupe fadhila wakati mwanzo ulikataa fadhila zangu,” amesema Harmonize.