
KOCHA Msadizi wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze amesema wamepanga kuendeleza ubabe wao leo Jumamosi mbele ya Namungo wakitumia mbinu walizozipata za wapinzani wao walipocheza na Simba.
Kauli hiyo ameitoa wakati timu hiyo ikijiandaa kujitupa kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi katika mchezo wa ligi dhidi
ya Namungo FC.
Kabla ya leo kuvaana na Yanga, Namungo walicheza na Simba wakati timu hiyo ikiwa chini ya Kaimu Kocha
Mkuu, Mnyarwanda Thierry Hitimana katika Uwanja wa Mkapa, Dar na kupoteza kwa bao 1-0.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaze alisema kuwa licha ya ugumu wa mchezo huo dhidi ya Namungo lakini watapambana kuhakikisha wanashinda na kuendelea kukaa kileleni.
Kaze alisema kuwa, watavaana Namungo wakiwa wanajua mbinu na wachezaji hatari wa kuchungwa katika
mchezo huo baada ya benchi la timu hiyo chini Koha Mkuu, Nasreddine Nabi kuona video ya mchezo wa ligi dhidi ya
Simba.
Aliongeza kuwa Namungo siyo timu ya kuidharau licha ya kufungwa dhidi ya Simba, inacheza kwa kujilinda na
kumiliki mpira muda mrefu.
“Kama benchi la ufundi tumekuwa na utaratibu wa kuwafuatilia wapinzani wetu kwa kutumia video za mwisho
za mchezo waliocheza kwa lengo la kuwajua vizuri wapinzani kwa maana ya mbinu na mfumo.
“Kikubwa tulichogundua ni timu nzuri yenye uwezo wa kujilinda na kukaa na mpira. Tuliwaona mechi
dhidi ya Simba walivyokuwa na uwezo kujituma muda wote uwanjani.
“Hivyo tunatakiwa kuwa makini nao katika kuhakikisha tunapata ushindi dhidi yao kesho (leo) tutakapokutana
nao.
“Tunataka kuona tunaendeleza ushindi wa mfululizo kwa kutoharibu rekodi yetu ya ushindi wa mfululizo, hilo
linawezekana kutokana na maelekezo, mafunzo ambayo tumewapatia,” alisema Kaze.
STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam