
IKIWA amekaa na timu kwa takribani siku nne, tayari kocha mpya wa Simba raia wa Hispania, Pablo Franco ameonesha wazi kuwa analijua tatizo la timu hiyo na fasta ameanza kulitibia.
Kwenye mazoezi yake ya kwanza Uwanja wa Boko Veteran, Dar, Ijumaa ya wiki iliyopita na kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanjani hapo Jumamosi, Spoti Xtra lilimshuhudia, Pablo akikomaa na vitu viwili, pasi nyingi na kufunga mabao ya kutosha.
Pablo hataki wachezaji wakae sana na mpira, badala yake unagusa moja, unaachia, ukiitaka tena unapewa, huku ukiwa unasogea kwenda kwenye eneo la timu mpinzani kushambulia.

Katika mazoezi ya Ijumaa, Jimmyson Mwanuke alikuwa nyota wa mchezo kwa kufunga mabao matatu ambayo yalipatikana kwa mtindo wa pasi nyingi, huku Ousmane Pape na Jonas Mkude wakinoga kwenye kugusa mpira na kuuweka kwenye njia kusaka mabao.
Kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa Jumamosi dhidi ya vijana wa Cambiaso ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, Simba walionekana kuwa na utofauti kuanzia kwenye kupanga mashambulizi na kutengeneza nafasi.

Mbali na Pablo kuonekana kusisitiza zaidi kwenye kumiliki soka na kupiga pasi za haraka, aliwataka wachezaji kuwa na haraka na spidi ya kufanya maamuzi wakati wanatengeneza mashambulizi.
Pablo anasaidiwa kwa ukaribu na wasaidizi wake wawili, Suleiman Matola na Hitimana Thiery raia wa Rwanda.
STORI: ISSA LIPONDA, Dar