×

Sakata la Mgao wa Umeme, Makamba Aanza Doria

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameanza doria katika mito inayoingiza maji katika mabwawa ya vituo vyote vya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji.

 

Katika doria hiyo, Waziri Makamba aliambata na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande na viongozi waandamizi wa TANESCO Doria hiyo ililenga kutathmini hali ya ukame katika mito hiyo, kiwango cha maji katika mabwawa, hali ya uzalishaji katika vituo hivyo, na kutathmini hatua za kuchukua kukabiliana na hali hiyo.

 

Waziri Makamba alishuhudia mtiririko hafifu katika Mto Ruaha na kukauka vya mito midogo inayochangia katika mtiririko wa mto Ruaha na katika bwawa dogo la Kidatu.

 

Hali hiyo imesababishwa na ukame mkali unaotokana na kutonyesha mvua katika maeneo yanayolisha mito hiyo na pia matumizi mabaya ya rasilimali-maji na uharibifu wa mazingira katika maeneo husika.

 

Hali hii imesababisha upungufu wa Megawati 307 kati ya Megawati 561 zinazopaswa kuzalishwa kutokana na nguvu ya maji. Waziri Makamba pia alipata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi katika vituo vya kuzalisha umeme, pamoja na wananchi na viongozi mbalimbali katika maeneo hayo.

 

Akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na viongozi mbalimbali katika maeneo husika, Waziri Makamba alisema kwamba ni dhahiri kwamba kuna ukame mkubwa ambao umeathiri mtiririko wa maji na hivyo kuathiri uzalishaji wa umeme.

 

Alisisitiza umuhimu wa hifadhi ya mazingira na matumizi ya rasilimali-maji yanayozingatia Sheria mbalimbali za nchi na hifadhi ya mazingira. Alisema kwamba TANESCO na Serikali zinachukua hatua za muda mfupi, wa kati na muda mrefu kukabiliana na upungufu wa umeme.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Ndugu Maharage Chande, aliongeza kwamba Shirika linachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia, kwa kuharakisha matengezo ya baadhi ya mitambo yake ya Ubungo I (MW 25), Upanuzi wa Kinyerezi I (MW 185) na Ubungo III (MW 112).

 

Aidha, Shirika limelazimika kuwasha kituo cha kuzalisha umeme cha Nyakato (MW 36). Hatua hizi zitakazokamilika kwa hatua kuanzia Desemba, 2021 hadi Machi, 2022 zitasaidia kuongeza jumla ya MW 350 katika mfumo wa gridi ya Taifa.

Leave a Comment