×

Harmo wa Jana Siyo Huyu wa Leo

Ni zaidi ya miaka mitano tangu Harmonize atambulike rasmi kwenye Bongo Fleva. Ngoma iliyomtoa ni Aiyola iliyotoka siku ile ya Agosti 25, 2015.

Video ya ngoma hiyo ilifanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kutoka Novemba 6, 2015 ikiwa imeongozwa na Director Nick Roux.

 

Ni wazi kipaji cha Harmonize au Konde Boy Mjeshi kilionekana ni kikubwa na ndiyo sababu Lebo ya WCB Wasafi chini ya Diamond Platnumz haikuona taabu kutoa pesa kwa ajili ya kufanya video hiyo inayotajwa kuwa ya gharama kubwa kwa msanii ambaye bado hajulikani.

 

Kwa mujibu wa Diamond, Video ya Aiyola iligharimu shilingi milioni 39. Hata hivyo, uwekezaji uliofanyika hadi jina la Harmonize kuwa kubwa ndani na nje ya Bongo ni zaidi ya shilingi milioni 115.

Ngoma ya Aiyola ikawa kubwa na kuvutia wengi ndani na nje ya nchi, haikuwa ajabu pale msanii wa Nigeria, Kiss Daniel kuonekana akiimba ngoma hiyo.

 

Na huo ukawa mwanzo wa maisha mazuri kupitia muziki, kutoka maisha ya kubangaiza katika mitaa ya Kariakoo, Dar hadi kuwa staa mkubwa.

Mafanikio ya ngoma hiyo yalisababisha Harmonize kushinda Tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) zilizotolea Dallas, Texas nchini Marekani katika Kipengele cha Msanii Bora Chipukizi kwa mwaka 2016.

 

Lakini kabla ya Aiyola kutoka tayari Harmonize alikuwa amerekodi ngoma iliyokwenda kwa jina la Kidonda Changu ambayo haikufanya vizuri.

Ngoma hiyo ya Kidonda Changu ndiyo iliyomfanya Diamond kumuona Harmonize ni mgodi unaotembea.

 

Basi wimbo huo ukampa Harmonize nafasi ya kutumbuiza kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa moja na Diamond ndani ya Ukumbi wa Dar Live. Usiku wa kuamkia Juni 17, 2018, Harmonize alikuwa na shoo yake aliyoipa jina la Kusi Night iliyofanyika Dar Live ambapo alisindikizwa na wasanii kama Queen Darleen, Ben Pol, Country Boy n.k.

 

Diamond ambaye hakutangazwa kuwepo kwenye shoo hiyo, aliibuka ghafla akitokea Next Door Arena ambapo alimsindikiza Davido wa Nigeria kwenye shoo yake.

Ujio wa Diamond kwenye shoo hiyo ulimtoa Harmonize machozi, ghafla alishindwa kutumbuiza ngoma yao ya Bado na kuanza kulia.

 

Kilio hicho cha furaha ni kutokana hapo ndipo walikutana kwa mara ya kwanza na ndiyo sehemu alifanya shoo yake ya kwanza kubwa na Diamond.

 

Katika shoo hiyo wawili hao walitumbuiza ngoma mbili walizofanya pamoja ambazo ni Bado na Kwangwaru ambayo ndiyo ilikuwa kwenye kilele cha mafanikio yake. Ngoma hizo mbili ndizo zenye mafanikio makubwa zaidi kwenye muziki wa Harmonize.

 

Katika chaneli ya Harmonize video ya Kwangwaru ndiyo inaongozwa kwa kutazamwa zaidi, ikifuatiwa na ile ya Bado.

Wakati Kwangwaru inatoka, tayari Harmonize alikuwa amefanya kolabo na wasanii kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

 

Miongoni mwao ni Marina (Rwanda), Yemi Alade (Nigeria), Eddy Kenzo (Uganda), Emma Nyra (Nigeria), Willy Paul (Kenya), IYO (Nigeria), OmoAkin (Nigeria), Korede Bello (Nigeria), Sarkodie (Ghana) na wengine.

Kutokana na mafanikio hayo, haikuwa ajabu kwa msanii huyo kutajwa kuwa ni miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva wenye pesa nyingi.

 

Mwanzoni mwa 2018, Diamond akiongea na Kipindi cha The Playlist kilichokuwa kinaruka Times FM alisema Harmonize ni miongoni mwa wasanii ambao anajua wana pesa nyingi mno katika katika lebo yake kwa wakati huo.

Inadaiwa tayari Harmonize alikuwa ameshachukua sehemu ya pesa zake na kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya kampuni ya kutengeneza video ya Zoom Production ambayo kwa sasa inajulikana kama Zoom Extra.

 

Aliamua kufanya hivyo baada ya kuona wanatumia pesa nyingi kwenda nje ya nchi kutengeneza video kwa kampuni zenye vifaa vya kisasa vinavyoendana na mahitaji yaliyopo kwenye soko lenye ushindani.

Hata hivyo, mwishoni mwa 2019, Harmonize aliamua kuondoka WCB akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko.

 

Na hapo ndipo Kampuni ya Zoom Production ikahama kwenda Zoom Extra na kuzipa nguvu zile tetesi zilizodai Harmonize alikuwa sehemu ya umiliki wa kampuni hiyo.

Kuondoka kwake WCB ukawa ni mwanzo mpya wa Harmonize kupata changamoto nyingine kwenye muziki na kufikia mafanikio makubwa zaidi.

 

Aliondoka kwenye lebo hiyo akiwa tayari ametoa Extended Playlist (EP) iitwayo Afro Bongo akiwashirikisha Yemi Alade, Mr Eazi na Burna Boy.

Kuondoka WCB haikuwa kazi rahisi. Kwa mujibu wa Harmonize mwenyewe, ili kuvunja mkataba wake wa miaka kumi na lebo hiyo ilimlazimu kulipa shilingi 500 kisha akaongezea shilingi milioni 100; jumla milioni 600 ili awe huru.

 

Usiku wa uzinduzi wa albam yake ya Afro East, Machi 14, 2020 aliulizwa na Mtangazaji Diva kama tayari amelipa pesa hizo. Jibu la Harmonize lilikuwa ameshamaliza deni ambalo awali alidai lilisababisha kuuza nyumba zake tatu.

Hilo likapita na uzinduzi wa albam hiyo ukachukua nafasi yake, huku Rais Mstaafu, Jayaka Kikwete akiwa mgeni rasmi akisikiliza wimbo wa kwanza hadi wa mwisho.

 

Miongoni mwa wasanii walioshirikishwa kwenye albam hiyo ni Burna Boy, Mr Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Khaligraph Jones, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr Eazi, Falz na wengineo.

Kilichofuata baada ya hapo ni Harmonize kuanza kusaini wasanii katika lebo yake, Konde Music Worldwide aliyoianzisha baada ya kuondoka WCB.

 

Ibraah ndiye alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa na kuachia EP yake iitwayo Steps kisha akafuata Country Boy ambaye naye aliachia EP, The Father kisha wakafuata wengine, Young Skales, Cheed, Killy na Anjella.

 

Kufika Novemba 5, 2021 Harmonize akaachia albam yake ya tatu, High School yenye nyimbo 20 ambazo amewashirikisha wasanii sita pekee ambao ni Anjella, Ibraah na Sholo Mwamba, wote kutoka Tanzania, wengine ni Sarkodie (Ghana), Naira Marley (Nigeria) na Busiswa (Afrika Kusini).

MAKALA; BAKARI MAHUNDU, BONGO

Makala; Sifael Paul, Bongo

Leave a Comment