
WATU wasiojulikana wametelekeza bastola aina ya Browing katika choo cha bar moja huko katika kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro ikiwa ni sehemu ya kutii sheria bila shuruti na agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani kutaka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuziwasilisha katika vituo vya jeshi la polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu amesema bastola hiyo yenye namba CZ 92 CAI 35 na usajili TZ CAR 88604 ilikuwa na risasi moja katika magazini na ilikutwa imetelekezwa katika moja ya maeneo ya kuuza vinywaji (bar).
“Tunasisitiza utekelezaji wa maagizo ya mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ya kuwataka wote wenye silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha silaha hizo,” anasema Kamanda Musilimu. Nakuongeza Bastola hiyo ilitelekezwa Novemba 13, mwaka huu (2021) majira ya saa 2: 30 usiku.