
Ni fursa ya kipekee kujivinjari katika jiji la Dubai! Ndivyo unavyoweza kutafisiri kile kinachosubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi ambapo jumla ya tiketi tano zimetolewa kwa ‘couple’ zitakazojishindia tiketi hizo.
Tiketi hizo zinatolewa Serikali ya jiji la Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo imefungua milango kwa Watanzania kushiriki tamasha la muziki, utamaduni pamoja na kufurahia vivutio vya utalii vya jiji hilo kwa kuwapatia tiketi za bure pamoja na za bei nafuu.

Tamasha hilo lililopewa jina la ‘AfroZons Dubai Soundoff ni mradi ambao umeratibiwa na Serikali ya Dubai kupitia Kituo cha Biashara, Masoko na Utalii (Dubai Tourism) kwa kushirikiana na Umoja wa Watangazaji maarufu wa radio wenye asili ya Afrika kutoka nchini Marekani (Afrozons Radio).
Katika tamasha hilo kwa upande wa Afrika litaratibiwa na watangazaji kutoka nchi za Nigeria, Ghana, Kenya, Tanzania, Angola, Zambia ambao kila mmoja ataungana na wasikilizaji wake kuelekea Dubai kwa safari ambayo imelipiwa kila kitu.

Akifafanua kuhusu mradi huo jana jijini Dar es Salaam, Mtangazaji wa kituo cha Redio cha Clouds Fm, Meena Ally ambaye ndiye mwakilishi kutoka Tanzania aliyechaguliwa kushiriki tamasha hilo, amesema Afrozons inalenga kuutangaza muziki wa Afrika yaani Afrobeat.
Aidha, amesema kila mtangazaji wa nchi hizo atapata nafasi ya kwenda Dubai lakini atapata nafasi ya kugawa tiketi tano ambazo zinawawezesha wasikilizaji wake kufika Dubai.

Ameongeza kuwa tiketi hiyo moja itatoa nafasi kwa watu wawili mathalani na mwenza wake na kukaa nchini humo kwa muda wa siku sita.
Amesema tiketi hizo zitafadhili safari nzima kuanzia usafiri, chakula, malazi, visa na matukio mbalimbali yatakayokuwa yanafanyika katika eneo hilo kama kutembelea vivutio mbalimbali.

Lakini kuna kampuni za usafiri wa anga Tanzania zimechaguliwa kutoa huduma ya usafiri kwa watu mbalimbali kuelekea Dubai kwa bei punguzo ambapo kwa safari ya mtu mmoja itakuwa kama dola za Marekani 450 hadi 500, lakini pia watapata fursa ya kutembelea maonesha makubwa ya kibiashara nchini humo yanayofahamika kama Dubai Expo2020.

Amesema washindi watano watakaoiwakilisha Tanzania, bado hawajatangazwa kwani tarehe ya kuelekea nchini humo ni kuanzia Machi 3 hadi 9 mwaka 2022.
Akifafanua namna washindi wanavyoweza kupatikana, alisema kwanza wanatakiwa kwenda kwenye tovuti ya Afrozons na kufungua sehemu iliyoandikwa give up, kisha win achieve in Dubai ambapo kuna fomu ambayo atajaza taarifa zake.

Aidha, mmoja wa wadau wa utalii nchini, Fahad Rajab Mwajasho ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya utalii wa ndani – Unzip Tanzania, ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa hiyo kutokana na bei punguzo ya tiketi iliyotolewa na Ufalme wa nchi za kiarabu
Ofisa Mtendaji wa Kituo cha Biashara, Masoko na Utalii (Dubai Tourism), Issam Kazim amesema zaidi ya watu 1500 watashiriki tamasha hilo.