
MBUNGE wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amesema hataondoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama ambavyo watu waekuwa wakimsema kwani anaamini anachokifanya (mafunzo yake ya cha Shule ya Uongozi) kiko sahihi kwa mujibu wa sheria.
Polepole amesema hayo leo Jumamosi, Desemba 11, 2021 wakati akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa LRHC, Kijitonyama, Dar es Salaam.
“Sijasema Serikali haifanyi kazi, Serikali inafanya kazi nzuri sana lakini ni jukumu letu na kukumbushana. Unadhani kwa nini malaria haiishi na tumesoma mpaka madarasa tukayamaliza? Halafu tunasema tu lete net, hivyo viwanda wanatengeneza wapi?, vya msaada.
“Nilipofanya Shule ya Uongozi nikapigiwa simu na watu wanaambiwa acha kwanza, nikauliza kwa nini? hakuna majibu. Nimefanya kazi na Mzee Mkapa, Kikwete, Magufuli na Mama Samia, hawa viongozi wangu wote hawajawahi kuniambia ‘kaa kimya’, nawashangaa wanaotaka ninyamaze.
“Mwalimu Nyerere alisema ‘hoja ahipigwi rungu, inajibiwa kwa hoja bora zaidi’, mimi ni mwana-CCM ninawaambia hapa kuna tatizo linarekebishika hivi, unasema kaa kimya, hilo ni jibu la hoja nilililoitoa. Niliitwa kwenye chama kwa tuhuma, nilizijibu zote moja baada ya nyingine, siwezi kusema, chama kitakuja kuzungumza.
“Hakuna Serikali mpya madarakani, Ilani walioinadi Ndugu Magufuli na Mhe. Samia 2020 ikatupa ushindi wa zaidi ya 84% ni ile ile, sera na mwelekeo wa Serikali ni ule ule, hakuna ilani nyingine mpya mpaka 2025. Ameondoka mtu mmoja tu, Magufuli sisi wengine wote tupo.
“Kuna watu wanasema Polepole anajitoa CCM anakwenda kuanzisha chama chake, nataka niwaambie niliingia CCm kwa hiari mwaka 2000 nikapiga kura kwa mara ya kwanza, sitatoka CCM kwa hiari. Kama ninatoka CCM washike wanitupe nje, bado tupo sana hapa,” amesema Polepole.