×

Fahamu Vigezo kwa Wanaotakiwa Kulipa Kodi – Video

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetolewa ufafanuzi kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawatakiwi kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria na wafanyabiashara wa kati na wakubwa wanaotakiwa kulipa kodi.

 

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Desemba 15, 2021 na Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi (TRA), Richard Kayombo wakati akizungumza mambo mbalimbali yahusuyo ulipaji kodi kupitia Kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio.

 

“Wafanyabiashara wadogo wasio na uwezo wa kutunza kumbukumbu ya mahesabu ya biashara zao, hawalazimiki kutengeneza mahesabu kwa ajili ya kukokotoa kodi, bali tunafanya mazungumzo ya makadilio ya mauzo/mapato yao.

 

“Kwa wafanyabiashara wadogo, kianzio cha chini cha kodi ni Tsh 100,000 ambacho analipa kwa awamu nne kwa mwaka. Level ya pili ni Tsh 250,000, kodi itapanda kulingana na ukubwa wa biashara yako.

 

“Kwa mfanyabiashara ambaye mauzo yake (sio mtaji) hayafiki Tsh milioni 4 kwa mwaka huyo hapaswi kulipa kodi, mfano wamachinga, mlipakodi lazima awe na anuani ya anapofanyia biashara yake, sio leo yuko hapa kesho kule.

 

“Mfanyabiashara mwenye mauzo kuanzia Tsh milioni 100 kwa mwaka huyu anaingia kundi la kati, na analazimika kutengeneza mahesabu yanayoonyesha manunuzi yake, gharama za uendeshaji, mauzo na faida. Atatozwa kodi kulingana na faida aliyopata.

 

“Ukitunza kumbukumbu huwezi kuwa na ugomvi na TRA, ndio maana tunasisitiza wanaotakiwa kuwa na EFD wawe nazo, ikifika wakati wa kukadiria wala hatubishani, kila kitu kinakuwa wazi.

 

“Kama wewe kwenye manunuzi yako umelipa VAT nyingi zaidi kuliko uliyopokea, Serikali itakukurejeshea hiyo tofauti, kama umepokea VAT nyingi kuliko ulizolipa, unatakiwa uilipe Serikali tofauti ya kiasi hicho, mwisho wa kulipa VAT ni tarehe 20 kila mwezi.

 

“Kodi haitozwi kutokana na mtaji, kodi inatozwa kutokana na faida ya biashara yake. Mtaji si kigezo cha ukubwa wa biashara, tunaangalia mauzo na tunalazimika kutembelea biashara yako kujiridhisha, lengo la Serikali si kumuonea mfanyabiashara bali kukusanya kwa haki,” amesema Kayombo.

 

Leave a Comment