
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha inayosikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imepokea gari aina ya Land cruiser alilouziwa Sabaya na shahidi wa kumi na mbili Sabri Sharif ambaye ni mfanyabiashara wa magari kama kielelezo cha ushahidi mahakamani hapo.
Shahidi wa 12 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, amedai mahakamani kuwa Februari 2, mwaka huu alimuuzia Sabaya gari hilo kwa fedha taslimu Tsh milioni 60.

Sharif Abdallah Shahibu (36) mkazi wa Dar es Salaam, alidai mahakamani kuwa alimuuzia Sabaya gari lenye namba za usajili T 222 BDW aina ya Toyota Land Cruiser. Kijana huyo mfanyabiashara ya magari anayemiliki Kampuni ya Sharja Motors alidai hayo wakati akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda.
Shahidi huyo mkazi wa Ilala, alidai biashara ya kumuuzia gari Sabaya ilifanyika katika nyumba za makazi za Black Hood, Kijitonyama mkoani Dar es Salaam. Aliiomba mahakama ipokee mkataba huo kama kielelezo katika kesi hiyo. Mawakili wa utetezi hawakuwa na pingamizi kuhusu kielelezo hicho kuwa moja ya ushahidi.
Shahidi Shahibu aliwatambua baadhi ya watu zaidi ya sita waliokuwepo siku hiyo ya kuuziana gari akiwemo Sabaya, mshitakiwa wa tatu na mshitakiwa wa tano ambao aliwagusa kwa kuwashika bega mbele ya Hakimu Kisinda.
Alidai awali gari hiyo aliiuza kwa Philipo Njombe kwa Sh milioni 90, lakini Njombe alilipa Sh milioni 70 na kubaki Sh milioni 20 alizoshindwa kumalizia na gari kuamua kumuuzia Sabaya, baada ya Njombe kulipwa Sh milioni 39, dalali Sh milioni moja na yeye alilipwa Sh milioni 20 na mkataba uliandaliwa na wakili wa Sabaya kwa gharama ya Sh 700,000.
Alidai alishughulikia uhamisho wa kadi ya gari kutoka Kampuni ya Magari ya Oil Com isomeke kwa jina la Lengai Ole Sabaya kwa gharama ya Sh 700,000, lakini alilipwa Sh 500,000 na hadi leo hajalipwa kiasi kilichobaki pamoja na jitihada za kuwatafuta bila ya mafanikio. Shahibu aliiomba mahakama ipokee kadi ya gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 222 BDW kuwa sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo.

Mawakili wa utetezi walipinga kupokelewa kwa kielelezo hicho kwa madai kuwa tarehe ya makabidhiano na alichosema mahakamani vinatofautiana. Kweka alikuwa na waendesha mashitaka wengine wa Jamhuri ambao ni Felix Kwetukia, Tasila Asenga, Othmed Mtenga, Neema Mbwana na Janet Segule na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mosses Mahuna, Faudhia Mustapher, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka na Fridorini Bwemelo.
Baada ya maelezo hayo, mahakama iliahirishwa kwa muda ili kupitia maelezo hayo na kuamua iwapo ipokee gari hilo ama la. Lakini baada ya kurejea katika maamuzi, mahakama imekubali kulipokea gari hilo.