
Jeshi la Polisi nchini Kenya, limewaua kwa kuwapiga risasi watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, katika majibizano ya risasi yaliyotokea katika Mji wa Ruaka, Kaunti ya Kiambu nchini humo.
Mkuu wa Kitengo cha The Special Service Unit (SSU), Pius Gitari ameliambia Gazeti la The Standard kwamba tukio hilo limetokea Jumanne ya Desemba 14, 2021 majira ya saa 10:15 asubuhi ambapo polisi waliwatilia shaka watu hao katika Kituo cha Mabasi cha Ruaka na kuwaamuru kusimama.
Kamanda Gitari ameongeza kuwa watu hao waliokuwa ndani ya gari aina ya Toyota Probox walikaidi amri hiyo na kuanza kufyatua risasi ambapo askari mmoja alijeruhiwa na baadaye, waliwazidi nguvu na kuwaua kwa risasi katika majibizano hayo.
Ameongeza kuwa baada ya upekuzi, walikutwa na bastola moja na risasi tano ambapo taarifa za kiintelijensia zinaonesha kwamba walikuwa kwenye mipango ya kuvamia jengo moja la kibiashara katika Mji wa Ruaka na kuongeza kuwa miili yao imehifadhiwa katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti katika Hospitali ya Ruaka.